Sera za kuingilia kati za Macron nchini Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63692-sera_za_kuingilia_kati_za_macron_nchini_lebanon
Matukio ya Kisiasa ya hivi karibuni nchini Lebanon hususan baada ya mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari ya Beirut mwezi Agosti mwaka huu ambao umepelekea kujiuzulu serikali ya nchi hiyo yametayarisha mazingira ya uingiliaji wa nchi za Magharibi hususan Ufaransa na Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 28, 2020 06:02 UTC
  • Sera za kuingilia kati za Macron nchini Lebanon

Matukio ya Kisiasa ya hivi karibuni nchini Lebanon hususan baada ya mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari ya Beirut mwezi Agosti mwaka huu ambao umepelekea kujiuzulu serikali ya nchi hiyo yametayarisha mazingira ya uingiliaji wa nchi za Magharibi hususan Ufaransa na Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Jumapili ya jana alikutana na waandishi wa habari na kuzungumzia tena matukio ya sasa ya Lebanon. Katika sehemu moja ya matamshi yake, Macron alisema kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya maafisa wa serikali ya Lebanon vimevuruga hali ya ndani ya nchi hiyo. Matamshi hayo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa yametolewa kwa kutilia maanani jitihada zinazofanya na Marekani katika kipindi hiki nyeti ikitaka kutumia hali hiyo kuishinikiza Beirut kwa ajili ya kudhamini maslahi ya tawala haramu wa Israel na vilevile kunufaika na hali hiyo katika kampeni za uchaguzi wa rais kwa maslahi ya Donald Trump. 

Sambamba na hayo Emmanue Macron mwenyewe amefuata mkondo huo huo wa kuingilia masuala ya ndani ya Lebanon. Rais huyo wa Ufaransa alisema kuwa hali mbaya ya sasa ya Lebanon haijawahi kushuhudia baada ya vita vya ndani vya nchi hiyo na kuongeza kuwa: Tabaka la mafisadi wa kisiasa linadhibiti madaraka ya Lebanon na maafisa wa serikali ya nchi hiyo hawatekelezi majukumu yao. Macron amesema kuwa, makundi ya kisiasa ya Lebanon katika Ikulu ya Baabda waliahidi kuwa wataunda serikali mpya katika kipindi cha siku 15. Nukta muhimu iliyoashiriwa katika matamshi ya Macron ni ukosoaji wake wa hali ya sasa ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Rais huyo wa Ufaransa amedai kuwa: "Hizbullah haiwezi kuwa jeshi linalopigana na Israel, kundi lenye silaha linalopigana vita Syria na chama cha siasa ndani ya lebanon." Macron amedai kuwa Ufarasna haitaiacha mkono Lebanon na itaendeleza ramani ya njia iliyochorwa. 

Macron na waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Saad Hariri

Matamshi hayo ya Rais wa Ufaransa kuhusiana na Lebanon yanaweza kutazamwa kwa njia mbili tofauti. Kwanza ni kuwa katika upande mmoja kiongozi huyo amekosoa msimamo hasi wa Marekani kuhusu Lebanon kwa maana ya sera zake mbovu za kuweka vikwazo kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya kisiasa. Katika upande mwingine Emmanuel Macron mwenyewe pia ametumbukia katika sera hizo hizo kwa kuzungumzia Lebanon kwa lugha ya kikoloni na kutaka kulitwisha taifa hilo mitazamo na matakwa ya Ufaransa. Hapa kunajitokeza swali kwamba, ni kwa misingi gani Macron anajipa haki ya kusimamia masuala ya Lebanon na kujivika gwanda la mtawala wa nchi hiyo? Inaonekana kuwa, Emmanuel Macron na kwa kutumia mitazamo ya kikoloni amejipa haki ya kutoa amri, kuainisha sera na kuamuru nini la kufanya na kipi cha kuacha nchini Lebanon kwa kutumia sera na misimamo ileile ya kikoloni. Kiongozi huyo amepuuza kabisa na kwa makusudi nafasi muhimu ya harakati ya Hizbullah katika kuzuia na kubatilisha njama za utawala haramu wa Israel dhidi ya nchi hiyo na na katika siasa za ndani na masuala ya kijamii ya Walebanon.

Dokta Bilal al Qais ambaye ni mhadhiri wa sayansi ya siasa nchini Lebanon ameashiria uingiliaji kati wa Marekani na Saudi Arabia katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kusema: Inaonekana kuwa, mbinu za Ufaransa zinatofautiana na zile za Marekani lakini malengo yao yanafafa. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, Ufaransa haiwezi kutengana na Marekani.

Hapana shaka kuwa mbinu ya Macron inalenga kuimarisha zaidi mrengo wa Magharibi nchini Lebanon na kudhoofisha kambi ya muqawama husan harakati ya Hizbullah.