Imran Khan asisitiza tena: Pakistan haitaitambua Israel wala kuanzisha uhusiano nayo
Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amekanusha kuwepo mashinikizo ya aina yoyote ya kuitaka nchi hiyo ijiunge na safu ya nchi zinazofanya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Imran Khan ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Pakistan ya SAMAA News alipozungumzia tetesi za kuwepo mawasiliano kati ya serikali ya Islamabad na Israel au kufanya safari waziri mmoja wa serikali hiyo kuelekea Tel Aviv na akasisitiza kwamba, huo ni uvumi tu na habari za kubuni zinazotolewa siku hizi na adui ili kuzipotosha fikra za waliowengi.
Kiongozi huyo wa chama tawala cha Pakistan Tehreek-e-Insaf vilevile amesema, ripoti kwamba serikali ya Islamabad inashinikizwa na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu hususan wa Saudi Arabia iukubali mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni hazina msingi wowote na akasisitiza tena kwamba Pakistan haitautambua utawala huo unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu.

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema, wananchi wa Pakistan wako bega kwa bega na wananchi wa Palestina na wanawaunga mkono kikamilifu katika kuhakikisha wanarejeshewa haki zao.
Mara kadhaa, wananchi wa Pakistan wamefanya maandamano makubwa kulaani jinai za utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel za kuwaua wananchi madhulumu wa Palestina na kutangaza uungaji mkono wao wa kudumu kwa malengo matukufu ya Wapalestina na kudhihirisha chuki na ghadhabu zao kwa Wazayuni maghasibu.../