Badran: Israel inaogopa ushindi wa Hamas katika uchaguzi ujao
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68134-badran_israel_inaogopa_ushindi_wa_hamas_katika_uchaguzi_ujao
Mwanachama mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeingiwa na kiwewe na wahaka mkubwa ukifahamu vyema kuwa harakati hiyo ya muqawama itaibuka mshindi katika uchaguzi ujao wa Palestina hususan katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2021 04:12 UTC
  • Badran: Israel inaogopa ushindi wa Hamas katika uchaguzi ujao

Mwanachama mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umeingiwa na kiwewe na wahaka mkubwa ukifahamu vyema kuwa harakati hiyo ya muqawama itaibuka mshindi katika uchaguzi ujao wa Palestina hususan katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika la habari la "Falastin al Yaum" limemnukuu Hussam Badran, mwanachama wa ngazi ya juu wa Hamas akisema hayo na kuongeza kuwa, utawala haramu wa Israel ndio wa kwanza kufaidi na migawanyiko na mizozo baina ya makundi ya Palestina.

Amebainisha kuwa, jitihada zozote za kujaribu kuziba mwanya uliopo baina ya makundi ya Kipalestina na kuyaleta pamoja makundi hayo ni tishio kubwa kwa utawala huo pandikizi.

Badran amesisitizia haja ya makundi yote ya Palestina kuungana na kuzungumza kwa sauti moja kuhusu kadhia ya uchaguzi unaotazamiwa kufanyika nchini humo karibuni hivi. Uchaguzi wa Bunge wa Palestina umepangwa kufanyika tarehe 22 mwezi Mei mwaka huu, uchaguzi wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina tarehe 31 mwezi Julai na ule wa Baraza la Taifa la Palestina tarehe 31 Agosti mwaka huu. 

Nembo ya Hamas ya Palestina

Hivi karibuni, makundi ya Palestina yalitoa taarifa mwishoni mwa kikao chao huko Cairo mji mkuu wa Misri yakikisisitizia kufanyika uchaguzi na kuunda chombo kimoja cha uongozi.

Yalisisitiza wajibu wa kulindwa umoja wa kisheria na kisiasa wa ardhi za Palestina na ulazima wa kufanyika uchaguzi huko Quds, Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza na kukabiliana na ukwamishaji wa aina yoyote wa utawala wa Kizayuni katika uwanja huo.