Wabunge 172 Iraq watia saini mpango wa kutaka bunge livunjwe
Mirengo kadhaa ya Bunge la Iraq imewasilisha mpango wa kutaka bunge hilo livunjwe ili kufanyike uchaguzi wa mapema.
Kwa mujibu wa tovutu ya Middle East News, wakuu wa mirengo kadhaa ya Bunge la Iraq jana Jumapili walishiriki katika mkutano na waandishi habari na kutoa taarifa ya pamoja. Katika taarifa yao, viongozi hao wa kisiasa wanasema kwa mujibu wa kipengee cha 64 cha katiba ya Iraq, inawezekana kuvunjwa bunge iwapo thuluthi moja ya wabunge watawasilisha ombi. Wameongeza kuwa, ifikapo Oktoba 9 2021, wabunge 172 watawasilisha mpango wa kuvunjwa bunge la Iraq.
Taarifa hiyo imesema mirengo mbali mbali ya kisiasa Iraq inaafikiana kuhusu kuvunjwa bunge na kwamba wawakilishi hao wa wananchi wanachukua hatua muhimu za kutaka uchaguzi wa mapema uitishwe.

Kati ya hatua ambazo bunge hilo linachukua kuelekea uchaguzi wa mapema ni kurekebisha sheria za uchaguzi, kuundwa timu huru ya uchaguzi ambayo itajumuisha wataalamu mashuhuri wa kisheria na wasomi wengine na pia kurekebisha sheria ya mahakama ya kifiderali.
Wakuu wa mirengo ya kisiasa katika bunge la Iraq wanasema kuitishwa uchaguzi wa mapema ni mwanzo wa duru mpya ya kisiasa nchini humo na kwamba mpango huo utajadiliwa katika kikoa kijacho cha bunge hilo.