Iraq na Syria zaendelea na mazungumzo kuhusu kurudi nyumbani wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68570-iraq_na_syria_zaendelea_na_mazungumzo_kuhusu_kurudi_nyumbani_wakimbizi
Nchi mbili za Iraq na Syria zinaendelea na mazungumzo baina yao kuhusu namna ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa nchi hizo mbili waliokimbilia katika nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 02, 2021 06:34 UTC
  • Iraq na Syria zaendelea na mazungumzo kuhusu kurudi nyumbani wakimbizi

Nchi mbili za Iraq na Syria zinaendelea na mazungumzo baina yao kuhusu namna ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa nchi hizo mbili waliokimbilia katika nchi hizo.

Kwa mujibu wa televisheni ya al Alam, Hasan Makhlouf, waziri wa idara ya kieneo na mazingira wa Syria jana Alkhamisi alionana na Aywan Faiq Jabru, waziri wa uhamiaji na wahajiri wa Iraq mjini Damascus Syria na pande mbili zimesema kuwa uhusiano wa mataifa hayo ndugu ni wa muda mrefu sana na ni wa enzi na jadi.

Waziri Makhlouf wa Syria amesema kuwa nchi yake iko tayari kuwarahisishia wakimbizi wa Iraq njia zote za kurejea kiurahisi nchini kwao yakiwemo masuala ya usafiri, usalama na mahitaji yote yanayotakiwa kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo.

Aidha ameashiria kwamba sreikali ya Damascus imechukua hatua nyingi za kuwarahisishia wakimbizi wa Syria walioko Iraq kurejea nchini kwao na kuongeza kuwa, Syria imefungua milango yake ya kuweza wakimbizi wote wa nchi hiyo kurejea nchini kwao na kuandaliwa mazingira mazuri ya kuanzia maisha.

Wakimbizi wa Syria

 

Kwa upande wake, Waziri Jabru amesema, Iraq inatilia mkazo sana wajibu wa kuimarishwa ushirikiano wa nchi hiyo na jirani yake Syria kadiri inavyowezekana na kwamba Baghdad nayo inafanya juhudi zake zote kuwarahisishia njia wakimbizi wote wa Syria wanaotaka kurejea kwa hiari nchini kwao waweze kufanya hivi bila ya kizuizi chochote.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema kuwa, hivi sasa kuna wakimbizi zaidi ya milioni 5 wa Syria wanaishi katika jirani na nchi hiyo.

Amma takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa wakimbizi wa Iraq walioko Syria ni takribani milioni moja na nusu hadi milioni moja la laki 7 na wengi wao wako Damascus na katika viunga vya mji mkuu huo wa Syria.