Zarif: Utawala wa Kizayuni umekithirisha jinai
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i70042-zarif_utawala_wa_kizayuni_umekithirisha_jinai
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekithirisha jinai zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 12, 2021 03:32 UTC
  • Zarif: Utawala wa Kizayuni umekithirisha jinai

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema utawala wa Kizayuni wa Israel umekithirisha jinai zake.

Zarif ameyasema hayo leo asubuhi punde baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Syria, Damascus na kuongeza kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishadidi kuanzia Ijumaa iliyosadifiana na Siku ya Kimataifa ya Quds.

Zarif ameongeza kuwa, matukio ambayo ni nadra kushuhudiwa yamejiri katika Msikiti wa Al Aqsa na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na pia hatua ya utawala wa Israel ya kudondosha mabomu katika Ukanda wa Ghaza yote hayo ni mambo ambayo yamepelekea hali kuwa mbaya katika eneo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kusema: "Tuko katika hali ya kipekee kabisa na katika wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa Syria nimefika katika nchi hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wakuu wa Syria kuhusu matukio haya muhimu."

Aidha amesema Syria ina nafasi muhimu sana kama mojawapo ya nchi ambazo zina nafasi muhimu katika kuunga mkono muqawama na harakati za ukombozi wa Palestina.

Rais Bashar al Assad wa Syria

Zarif amesema akiwa Damascus atafanya mazungumzo kuhusu uchaguzi wa Syria na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa serikali na taifa la Syria katika ujenzi mpya wa nchi hiyo na pia vita dhidi ya ugaidi.

Aidha amesema atafanya mazungumzo na Rais Bashar al Assad wa Syria, Waziri wa Mambo ya Nje Faisal Mikdad na wawakilishi wa makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina ambapo watatathmini matukio ya hivi sasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.