Nukta sita kuhusu uchaguzi wa rais nchini Syria
Uchaguzi wa pili wa rais katika muongo mmoja uliopita nchini Syria ulifanyika jana Mei 26. Tunaweza kuashiria nukta kadhaa hapa kuhusu uchaguzi huo.
Nukta ya kwanza ni kuwa, katika uchaguzi huo, kuna wagombea watatu wanaowania nafasi ya urais. Katika duru hii ya uchaguzi Rais wa sasa Bashar al-Assad anashindana na naibu waziri wa zamani Abdullah Sallum Abdullah ambaye ni mwanachama wa Chama cha Muungano wa Kisosholisti na Mahmoud Ahmad Marei, ambaye ni mkuu wa Shirika la Kiarabu la Haki za Binadamu. Pamoja na hayo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Rais Bashar al Assad ndiye atakayeibuka mshindi kutokana na umashuhuri wake.
Nukta ya pili ni kuwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria imeandaa uchaguzi huo kwa njia bora huku kukiwa na usalama katika aghalabu ya maeneo ya nchi hiyo. Kuhusiana na nukta hii, Mohammad Khaled al-Rahmoun amesema kulikuwa na masanduku 12,102 ya kupigia kura katika miji na maeneo yote ya Syria. Kwa hivyo kufanyika uchaguzi katika kona zote za Syria kunahesabiwa kuwa ni mafanikio muhimu kwa mfumo unaotawala Syria.
Nukta ya tatu inahusu waliotimiza masharti ya kupiga kura. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria, idadi ya Wasyria waliotimiza masharti ya kupiga kura ndani na nje ya nchi hiyo ni milioni 18.
Nukta ya nne inahusiana na maeneo au jiografia ya upigaji kura. Upigaji kura umefanyika katika aghalabu ya maeneo yote ya kijiografia ya Syria. Hata hivyo hakukuwa na upigaji kura katika maeneo machache ambayo yanakaliwa kwa mabavu na Uturuki na wanamgambo wanaofungamana na Uturuki. Maeneo hayo ni kama vile Ras al Ain, Afrin na maeneo mengine ambayo wanayadhibiti. Aidha uchaguzi haukufanyika katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na magaidi mkoani Idlib. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Syria amesema ili Wasyria waweze kutekeleza haki ya kupiga kura, vituo maalumu vya kupigia kura vimewekwa karibu na maeneo yanayodhibtiiwa na magaidi au wanamgambo ili wananchi wanaotaka waweze kupiga kura. Nukta hii inaonyesha kuwa serikali ya Syria inalipa umuhimu suala la Wasyria kutekeleza haki yao ya kupiga kura na ina azma ya kukomboa maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na magaidi na waitifaki wao wa kigeni.
Nukta ya tano ni hii kuwa uchaguzi wa rais nchini Syria unafanyika katika hali ambayo tokea mwaka 2011 hadi sasa nchi hii ya Kiarabu imekuwa ikikabiliwa na njama za kimataifa ambazo zinatekelezwa kupitia hujuma ya magaidi wakufurishaji watenda jinai. Njama hizo zinazoendelea zimekuwa zikitekelezwa kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar Assad. Ni kwa kuzingatia nukta hiyo ndio maana nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zikadai kuwa uchaguzi wa sasa hauna uhalali. Propaganda hizo zimekuwa zikienezwa ili kupunguza kiwango cha ushiriki katka uchaguzi huo.
Nukta ya sita ni hii kuwa, kufanyika uchaguzi wa rais nchini Syria kwa mara ya pili katika muongo mmoja ni baraka inayotokana na kushikamana wananchi na viongozi na jeshi la nchi hiyo sambamba na uungaji mkono wa mhimili wa muqawama. Hivi sasa serikali halali ya Syria imebakia madarakani ikiwa imara kabisa na si tu kuwa imeshavuka hatari ya kuangushwa bali imeweza kufikia uthabiti wa kisiasa. Kushiriki kwa wingi wananchi wa Syria katika upigaji kura kuna maana ya kuwepo matumaini kuhusu kurejea maisha katika hali ya kawaida na Syria kupata tena hadhi katika uga wa kieneo.