Kuendelea mashambulizi ya jeshi la Uturuki Kaskazini mwa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71300-kuendelea_mashambulizi_ya_jeshi_la_uturuki_kaskazini_mwa_syria
Wanajeshi wa Uturuki wanaendeleza mashambulizi mtawala dhidi ya maeneo ya raia huko Iraq na Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 15, 2021 09:02 UTC
  • Kuendelea mashambulizi ya jeshi la Uturuki Kaskazini mwa Syria

Wanajeshi wa Uturuki wanaendeleza mashambulizi mtawala dhidi ya maeneo ya raia huko Iraq na Syria.

Inaonekana kwamba jeshi la Uturuki linazisadia harakati za makundi ya kigaidi za kigeni, haswa kundi la kigaidi la Daesh licha ya serikali ya Ankara kutoa nara za kupambana eti na makundi ya kigaidi katika nchi za Iraq na Syria. 

Katika mkondo huo jeshi la Uturuki limeshambulia ngome za wapiganaji wa kundi la YPG katika eneo la Tall Rifat huko Kaskazini mwa Syria. Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imedai kuwa, mashambulizi hayo yamefanyika kujibu mashambulizi ya mizinga yaliyofanywa juzi usiku ya wapiganaji vya YPG katika hospitali moja huko kaskazini mwa Syria.

Tangu yapata miaka mitatu iliyopita jeshi la Uturuki lilivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Uvamizi na mashambulizi hayo vimelaani na Wasyria na jamii ya kimataifa. Si hayo tu, bali hata nchi za Magharibi waitifaki wa Uturuki zinasema kuwa, uvamizi wa Ankara na kuzikalia kwa mabavu baadhi ya ardhi ya Syria na Iraq vinakiuka sheria za kimataifa.

Wanajeshi wa Uturuki kaskazini mwa Iraq

Wakati huo huo wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa shambulizi la karibuni la jeshi la Uturuki dhidi ya Wakurdi ambalo kidhahiri limefanyika kwa jina la kulinda usalama wa taifa wa nchi hiyo na kuliangamiza kundi la PKK, kwa hakika limefanyika kwa shabaha ya kukomboa wapiganaji elfu 20 ambao aghlabu yao ni raia wa nchi za Ulaya na Waarabu wanachama wa kundi la Daesh, wapiganaji wa kundi linalojiita jeshi la ukombozi wa Syia na kundi la Jabhatu Nusra. Brigedia Jenerali mstaafu wa jeshi la Syria, Haytham Hassun anasema: "Jeshi la Uturuki liliingia kwenye vita vya Syria likishirikiana na magenge ya kigaidi na limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Syria likiwemo lile la mji wa Saraqib na miji mingine ya Syria."

Mtaalamu huyo wa masuala ya kijeshi anasema, kipaumbele cha kwanza cha serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ni kuyasaidia makundi ya waaasi na magaidi katika ardhi ya Syria. Pamoja na hayo inatupasa kusema kuwa, kuwepo kwa mabavu majeshi ya Uturuki katika nchi za Syria na Iraq hakujaweza kutimiza malengo ya serikali ya Ankara. Maafisa wa serikali ya Uturuki wanafanya jitihada za kuyakalia kwa mababu milele baadhi ya maeneo ya nchi hizo mbili kwa kutumia kisingizio kwamba, Iraq na Syria ziko katika hali ya vita. Kwa maneno mengine ni kuwa, maafisa wa serikali ya Ankara wanataka kutimiza malengo yao maalumu katika nchi hizo kwa kuvamia ardhi ya nchi mbili zinazojitawala za Iraq na Syria. 

Vifaru vya jeshi la Uturuki nchini Syria

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, kwa kutilia maanani hali ya sasa ya Syria, ambayo inakabiliana na magengo hatari ya kigaidi yanayofadhiliwa na nchi za Magharibi na hadi sasa imefanikiwa kukomboa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, kwa sasa hakuna uwezekano wa kuwafukuza wanajeshi wa Uturuki waliovamia baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Hata hivyo inatupasa kuelewa kwamba, baada ya kukamilisha operesheni ya kuyaangamiza kikamilifu magenge ya kigaidi yanayosaidiwa na nchi za Kiarabu na Kimagharibi, Syria itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuyafukuza majeshi vamizi ya nchi za kigeni kama ya Uturuki na Marekani yaliyovamia nchi hiyo na hata kujenga kambi za kijeshi katika ardhi yake.