Mahmoud Abbas: Kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel hakuwezi kuleta amani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71830-mahmoud_abbas_kutangaza_uhusiano_wa_kawaida_na_israel_hakuwezi_kuleta_amani
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amejibu kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) cha kufungua rasmi ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini Abu Dhabi na kusema kuwa, makubaliano ya uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu na Israel kamwe hayawezi kuleta utulivu na amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2021 01:49 UTC
  • Mahmoud Abbas: Kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel hakuwezi kuleta amani

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amejibu kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) cha kufungua rasmi ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini Abu Dhabi na kusema kuwa, makubaliano ya uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu na Israel kamwe hayawezi kuleta utulivu na amani.

Mahmoud Abbas amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mkutano mmoja wa kielimu uliofanyika Ramallah kwa usimamiaji wa Chuo Kikuu cha Quds.

Amesema, usalama na amani itapatikana tu baada ya kuondolewa uvamizi wa utawala wa Kizayuni kwenye ardhi za Wapalestina na kukombolewa haki zote za taifa hilo sambamba na kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas.

Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, dunia hivi sasa inashuhudia uhakika wa dola la Israel na inaona jinsi utawala huo ulivyo vamizi na mbaguzi za kizazi.

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umeendeleza usaliti wake kwa kadhia ya Palestina kupitia kufungua rasmi ubalozi wa utawala wa Kizayuni mjini Abu Dhabi jana Jumanne.

Njia pekee ya kukomboa ardhi za Palestina ni mapambano ya silaha

 

Kambi ya muqawama imekuwa ikisisitiza kuwa, kitendo cha Israel cha kuomba hifadhi kwa nchi ndogo na dhaifu kama Imarati, hakiwezi kuzuia kuporomoka kwake.

Makundi ya muqawama hasa ya HAMAS na Jihadul Islami huko Palestina yamekuwa yakisisitiza kuwa yataendelea kupambana kwa njia zote zikiwemo za kijeshi na kisiasa hadi zitakapokomboa ardhi zote za Palestina na kulipatia taifa hilo haki zake zote. 

Ubalozi wa Israel umefunguliwa huko Abu Dhabi Imarati wiki chache tu tangu baada ya vita vya siku 12 vya Ghaza ambapo katika vita hivyo, utawala wa Kizayuni uliua kikatili Wapalestina wasiopungua 256 wakiwemo watoto wadogo 67 wasio na hatia na kujeruhi zaidi ya 2000 wengine.