Bashar al Assad: Tunafanya jitihada ili wakimbizi wa Syria warejee nchini
(last modified Tue, 27 Jul 2021 07:22:11 GMT )
Jul 27, 2021 07:22 UTC
  • Bashar al Assad: Tunafanya jitihada ili wakimbizi wa Syria warejee nchini

Rais wa Syria amesisitiza kuwa Damascus inafanya jitihada kuandaa mazingita ya kurejea wakimbizi nchini.

Akizungumza na ujumbe kutoka Russia ulioongozwa na Alexander Lavrentiev Mjumbe Maalumu wa Rais Vladimir Putin wa Russia huko Damascus, Rais Bashar al Assad ameishukuru serikali ya Moscow kwa misaada yake ya kibinadamu kwa wananchi wa Syria, kufanya juhudi za kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Syria na kutuma nchini humo chanjo ya corona.  

Rais Assad amesema kuwa, serikali ya Syria inafanya kila iwezalo kurejesha amani na uthabiti katika maeneo yaliyokombolewa nchini ili kurahisisha kurejea haraka wakimbizi wa Syria katika miji na vijiji vyao. 

Katika mazungumzo hayo naye Alexander Lavrentiev amesema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana mtawalia na Syria ili kupunguza matatizo na changamoto zinazoikabili nchi hiyo na pia kuharakisha mchakato wa kurejea nchini wakimbizi. Amesema matarajio yake ni kuona Damascus na Moscow zinafikia natija ya maana katika nyanja zote. 

Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa, wakimbizi wa Syria karibu milioni sita wanaishi nje ya nchi. Wakimbizi hao wanaishi Uturuki, Jordan, Lebanon na Iraq.

Wakimbizi wa Syria katika kambi nchini Jordan