Walebanon wakaribisha hatua ya Hizbullah ya kuagiza mafuta kutoka Iran
Hotuba ya Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuhusu safari ya meli za mafuta kutoka Iran zinazoelekea nchini humo imekaribishwa kwa shangwe na wanasiasa na sehemu kubwa ya wananchi wa Lebanon hususan katika mitandao ya kijamii.
Sayyid Hassan Nasrullah alisema jana Alkhamisi kwenye hotuba yake ya maombolezo ya Ashura na siku ya kumbukumbu ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) kwamba, meli zinazobeba mafuta zitang'oa nanga kutoka Iran zikielekea Lebanon masaa machache yajayo.
Katibu Mkuu wa Hizbullah pia amezitahadharisha Marekani na Israel zisithubutu kushambulia meli hizo za mafuta kutoka Iran na kusisitiza kuwa, harakati hiyo ya mapambano inazitambua meli hizo kuwa ni sawa na ardhi ya Lebanon.
Hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa Hizbullah kuhusu kuiagiza shehena ya mafuta kutoka Iran imepongezwa na kuwafurahisha wananchi na wanasiasa wengi wa Lebanon isipokuwa idadi ndogo ya vyama vyenye mielekeo ya Kimagharibi.
Baada tu ya hotuba hiyo ya Sayyid Nasrullah, kiongozi mwenye mielekeo ya Kimagharibi wa chama cha al Mustakbal, Sa'ad Hariri alidai kuwa meli zinazobeba mafuta ya msaada kutoka Iran zinaandamana na hatari ya vikwazo zaidi kwa nchi ya Lebanon. Hariri pia amepinga matamshi ya Sayyid Nasrullah aliyesema kuwa meli hizo za mafuta ni sawa na ardhi ya Lebanon, ambayo haipaswi kushambulia na upande wowote.
Matamshi ya Hariri yamejibiwa na Wiam Wahhab, Mwenyekiti wa chama cha al Tauhid al Arabi ambaye amesema: Matamshi ya Hariri yanafunga mlango wa kuundwa serikali mpya nchini Lebanon. Wahhab amehoji kwamba, je, Hariri anataka kutumia safu ya madhila na kudhalilishwa kwa ajili ya kuwaridhisha mabwana zake wa Kimarekani?
Wakati huo huo watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Lebanon wamempongeza Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutuma shehena ya mafuta kuwasaidia wananchi wa Lebanon.
Nchi hiyo inasumbuliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na kisiasa kwa kipindi cha mwaka mzima sasa.
Mgogoro wa uhaba wa nishati na mafuta nchini Lebanon umekuwa mkubwa kiasi kwamba, habari zinasema umeme umekatwa katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi hiyo na mahospitalini.