Nafasi ya Marekani katika mgogoro wa sasa nchini Lebanon
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah Jumapili ya juzi tarehe 22 Agosti alitoa hotuba akizungumzia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kusema kuwa, Marekani imekuwa na nafasi kubwa katika kuchochea mgogoro wa sasa wa Lebanon.
Kwa sasa nchi ya Lebanon inasumbuliwa na migogoro mikubwa ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Migogoro ya nchi hiyo ina sababu na wachezaji kadhaa lakini wachambuzi wengi wa mambo ya ndani na nje ya Lebanon na Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah wanaamini kuwa, siasa za Marekani ndiyo sababu kuu ya changamoto zinazoikabili nchi hiyo kwa sasa. Sayyid Nasrullah ameashiria masuala manne kuhusu nafasi ya Marekani katika changamoto za sasa za Lebanon.
Kwanza ni kwamba ubalozi wa Marekani na balozi wa nchi hiyo mjini Beirut ni miongoni mwa wachezaji wakuu katika changamoto na migogoro ya sasa ya Lebanon. Marekani imekuwa na mtazamo makhsusi kuhusiana na Lebanon kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushawishi wa Hizbullah nchini humo na kupakana nchini hiyo na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Kwa sababu ya mtazamo huo, Marekani imekusudia kujenga ubalozi wake wa pili kwa ukubwa zaidi duniani nchini Lebanon baada ya ubalozi wa nchi hiyo huko Iraq. Mchambuzi na mwanastatejia mkubwa wa Lebanon, Amin Khatit nasema, hatua hiyo ya Marekani inazingatia zaidi masuala ya usalama kuliko ya kisiasa, na imepangwa kuwa, ubalozi huo wa Marekani utakuwa kituo kikuu cha usalama cha kudhibiti Beirut na kutoa huduma za kiusalama kwa Israel.
Kwa sababu hiyo, katika hotuba yake ya juzi Katibu Mkuu wa Hizbullah alisema: "Ubalozi na balozi wa Marekani mjini Beirut anaingilia masuala yote ya Lebanon kuanzia uteuzi wa maafisa wa serikali hadi kuchukua maamuzi yanayohusiana na nishati na mafuta."
Pili ni kwamba, ubalozi wa Marekani mjini Beirut umekuwa kituo cha kupambana na harakati ya mapambano ya Hizbullah ndani ya ardhi ya Lebanon. Kwa maneno mengine ni kuwa, sambamba na kuingilia masuala yote ya ndani ya Lebanon, mabalozi wa Marekani mjini Beirut wanaongoza na kusimamia harakati zote dhidi ya Hizbullah kupitia maajenti wao wa ndani ya nchi. Katibu Mkuu wa Hizbullah anasema: "Vita vilivyoanzishwa dhidi ya Hizbullah na makundi halisi ya kitaifa vinaongozwa ndani ya ubalozi wa Marekani mjini Beirut; na mabalozi wote wa Marekani kuanzia mwaka 2005 wamekuwa makamanda halisi wa vibaraka wanaoshiriki katika vita hiyo dhidi ya muqawama."
Tatu ni kwamba, hivi karibuni Marekani ilitoa pendekezo la kusafirisha umeme kutoka Jordan hadi Lebanon. Mpango huo ulipendekezwa mara tu baada Sayyid Hassan Nasrullah kutangaza Alkhamisi iliyopita kwamba, meli zinazobeba mafuta za Iran zimeong'a nanga kuelekea Lebanon. Lengo kuu la mpango huo wa Marekani ni kutaka kuvuruga mpango wa kupeleka shehena za mafuta ya Iran nchini Lebanon na kuendeleza propaganda chafu dhidi ya harakati ya Hizbullah na Jamhuri ya Kiislamu. Kwa upande mwingine Syria pia imeeleza msimamo wake kuhusiana na mpango huo, kwa sababu usafirishaji wa nishati kutoka Jordan hadi Lebanon unapaswa kupitia nchini Syria; hivyo Damascus nayo ina masharti yake kuhusiana na kadhia hiyo.
Nne ni kwamba, Marekani si tu kwamba haiisaidii Lebanon, bali pia inazuia misaada ya nchi nyingine kwa taifa hilo. Ukweli ni kwamba, Washington inataka kuona "Lebanon iliyo chini ya mashinikizo" na inakaribisha na kupongeza changamoto zote zinazoikabili nchi hiyo. Kwa sababu hiyo imeiwekea vikwazo Hizbullah na baadhi ya viongozi wake, na wakati huo huo umezighadhabikia nchi zote zinazoisaidia Lebanon.
Kwa kuzingatia hayo, katika hotuba yake ya juzi Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah alimhutubu balozi wa Marekani mjini Beirut akisema: "Kama unataka kuihudumia Lebanon iambie serikali ya nchi yako iache kuzuia misaada ya nchi nyingine kwa Lebanon. Sisi hatutaki mipango yako wala fedha za Marekani."