Aug 24, 2021 13:14 UTC
  • Mrengo wa Utawala wa Sheria Iraq: Mchakato wa kuondoka askari wa Marekani uharakishwe

Mrengo wa Muungano wa Utawala wa Sheria nchini Iraq unaoongozwa na waziri mkuu wa zamani Nouri al Maliki umetilia mkazo udharura wa kuharakishwa mchakato wa askari wa Marekani kuondoka nchini humo.

Mrengo wa Muungano wa Utawala wa Sheria leo umetoa taarifa ukimtaka Waziri Mkuu Mustafa Al Kadhimi, ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo aharakishe uandaaji wa ratiba ya kuondoka askari wa jeshi la Marekani nchini Iraq kulingana na tarehe na muda maalum.

Abdulhadi As-Saadawi, mbunge kutoka mrengo wa Muungano wa Utawala wa Sheria katika bunge la Iraq amesema, serikali inapaswa iandae jedwali la ratiba maalum kuhusiana na kuondoka askari walio chini ya muungano wa kimataifa wa kijeshi.

As-Saadawi amebainisha kuwa, mpango uliopitishwa na bunge la Iraq unafahamika vyema na kila mtu; na kwa mujibu wa mpango huo hakuna haja ya kuwepo askari wa kigeni kwa kisingizio chochote kile na kwamba Iraq haihitaji kuwepo askari wa Marekani katika ardhi yake.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa Al Kadhimi

Hayo yanaripotiwa wakati kabla ya hapo, Jasim Al-Bayati, mbunge wa zamani wa Iraq kutoka mrengo wa Muungano wa Utawala wa Sheria alisisitiza kwamba kwa mujibu wa mazungumzo aliyofanya Waziri Mkuu Mustafa Al Kadhimi na Rais Joe Biden wa Marekani mjini Washington, askari wote wa Marekani wataondoka nchini Iraq.

Askari wa jeshi vamizi la Marekani wamepiga kambi ndani ya ardhi ya Iraq tangu mwaka 2003, ilhali wananchi na makundi mbalimbali ya nchi hiyo wameshatoa miito mara kadhaa kuwataka waondoke, huku bunge la nchi hiyo pia likiwa limeshapitisha mpango kuhusu askari hao kuondoka nchini humo.../

Tags