Maandamano dhidi ya Pakistan mjini Kabul, Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i74620-maandamano_dhidi_ya_pakistan_mjini_kabul_afghanistan
Idadi kubwa ya wananchi wa Kabul mji mkuu wa Afghanistan wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Pakistan wakiitaka Islamabad iache kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2021 01:29 UTC
  • Maandamano dhidi ya Pakistan mjini Kabul, Afghanistan

Idadi kubwa ya wananchi wa Kabul mji mkuu wa Afghanistan wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Pakistan wakiitaka Islamabad iache kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.

Waandamanaji hao ambao wamepiga nara kama "Pakistan, Pakistan, toka Afghanistan" na "Tunataka Uhuru" wamelitaka kundi la Taliban liunde serikali bila ya uingiliaji wa Pakistan. Mikusanyiko kama hiyo imefanyika pia mbele ya balozi za Pakistan katika miji mikuu ya nchi tofauti dunaini. 

Licha ya kuweko mitazamo mbalimbali, lakini kufanyika maandamano mbele ya ubalozi wa Pakistan mjini Kabul tena kwa mipango maalumu ni jambo ambalo inabidi lipewe mazingatio makubwa. Sababu yake ni kuwa, hivi sasa Taliban ndio wanaoidhibiti Afghanistan. Kundi hilo linaungwa mkono kikamilifu na Pakistan. Hivi karibuni Taliban walionya kuhusu mikusanyiko yoyote isiyo na kibali cha mamlaka husika. Sasa ni vigumu kukubali kwamba maandamano makubwa yaliyofanyika mbele ya ubalozi wa Pakistan mjini Kabul yamefanyika vivi hivi tu kwa watu kujitokeza bila ya kuweko mipango maalumu ya kabla.

Baadhi ya viongozi wa kundi la Taliban

 

Hata tukikubali kwamba mazingira ya kufanyika mikusanyiko kama hiyo yalikuwa yameandaliwa mjini Kabul, lakini kuongezeka idadi ya waandamanaji mbele ya ubalozi wa Pakistan mjini humo na ambao wamepinga vikali uingiliaji wa Pakistan katika masuala ya ndani ya nchi yao na kuonesha hasira kubwa juu ya jambo hilo, ni jambo linaloleta utata, ijapokuwa wanamgambo wa Taliban walipiga risasi hewani kuwatawanya waandamanaji hao.

Hossein Naseri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Pakistan inaihesabu Afghanistan kuwa ndiyo sababu ya kubakia kwake katika mapambano yake na India na katika kulinda ukuta uliopo baina ya nchi hizo mbili. Lakini Afghanistan nayo inapinga uwepo wa nchi ya Pakistan kiasi kwamba huko nyuma iliwahi kupiga kura ya kukataa kuundwa nchi ya Pakistan ndani ya Umoja wa Mataifa.

Kiujumla ni kwamba hakuna anayeweza kukataa ukweli kuwa wananchi wa Afghanistan wanachukizwa na uingiliaji wa kigeni wa masuala yao ya ndani unaofanywa na nchi yoyote hasa Pakistan. Lakini Islamabad inaiona Afghanistan ni eneo lake la kujifaragua na kutamba na inaiangalia nchi hiyo kwa jicho pana sana la kiistratijia na ndio maana mara zote Pakistan ina hamu ya kuona kuna serikali kibaraka wake huko Afghanistan. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana, si wananchi wa Afghanistan tu, bali hata duru za kimataifa, mara kwa mara zimekuwa zikionya kuhusu madhara ya uingiliaji wa Pakistan katika masuala ya ndani ya Afghanistan. Shirika la kijasusi la jeshi la Pakistan ISI ndilo linalofuatilia kadhia ya  Afghanistan. Hata hayati Benazir Bhuto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan aliwahi kukiri kwamba kundi la Taliban ni zao la Pakistan kwa kushirikiana na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na nchi nyingine za Kiarabu za eneo hili. Hivyo kwa mtazamo wa wananchi wa Afghanistan, kudhibitiwa nchi yao na kundi la Taliban kuna maana ya kuingia kikamilifu Afghanistan, mikononi mwa Pakistan.

Shirika la kijasusi la jeshi la Pakistan ISI

 

Sayyid Abbas Hosseini, mtaalamu mwingine wa masuala ya kisiasa anasema: Wananchi wa Afghanistan kamwe hawatolikubali wala kuliamini kundi la Taliban na kundi jingine lolote, ila baada ya kuwathibitikia kuwa ni kundi la kitaifa na si kibaraka wa Pakistan au nchi nyingine.

Alaakullihaal, Pakistan inatambua vyema kwamba mazingira ya hivi sasa ya kudhibitiwa Afghanistan na kundi la Taliban ni tofauti kabisa na mazingira ya miaka 20 iliyopita. Wananchi wa Afghanistan hasa wanawake na kaumu na makabila mbalimbali, wamekuwa na maisha mengine kabisa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na hawako tayari kuona wanarejeshwa katika maisha ya miongo miwili nyuma. Ni wazi kuwa, nchi haiwezi kutawaliwa ikiwa na vurugu na ukosefu wa utulivu. Wanawake wana nafasi muhimu na kubwa ya kuleta utulivu katika jamii. Hamu ya wananchi wa Afghanistan ya kuwa na nchi iliyopiga hatua za kimaendeleo inayafanya mazingira ya hivi sasa yawe tofauti kabisa na miaka 20 iliyopita.