Interpol yairejeshea Syria uanachama wake
Syria imerejeshewa uanachama wake katika shirika la Polisi ya Kimataifa (Interpol).
Afisi ya Habari ya Interpol imeliambia shirika la habari la The New Arab kuwa, Damascus imeruhusiwa upya kutumia kanali salama za mawasiliano za taasisi hiyo ya kimataifa.
Interpol ndicho chombo kikubwa zaidi cha polisi duniani, chenye jukumu la kukabiliana na uhalifu wa kimataifa. Hivi sasa shirika hilo la kimataifa lina nchi wanachama 194.
Tangu mwaka 2011, Syria inashuhudia vita dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo vilivyoanzishwa na makundi ya kigaidi ya wapiganaji kutoka nchi zaidi ya 100 duniani yanayoungwa mkono na madola ya eneo na nje ya eneo, lengo likiwa ni kuiangusha serikali hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, kati ya Machi 2011 hadi Machi 2021 watu 350,209 wamebainika kuwa wameuawa katika mapigano nchini Syria.
Baada ya kushtadi mapigano nchini Syria, nchi hiyo ya Kiarabu ilivuliwa uanachama wa taasisi na mashirika mengi ya kieneo na kimataifa.