Kiongozi wa Taliban, Mullah Mansour auawa katika hujuma ya drone
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7579-kiongozi_wa_taliban_mullah_mansour_auawa_katika_hujuma_ya_drone
Kiongozi wa kundi la kigaidi la Taliban, Mullah Akhtar Mohammad Mansour ameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Marekani katika mkoa wa Baluchistan, mpakani mwa Afghanistan na Pakistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2016 11:50 UTC
  • Kiongozi wa Taliban, Mullah Mansour auawa katika hujuma ya drone

Kiongozi wa kundi la kigaidi la Taliban, Mullah Akhtar Mohammad Mansour ameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Marekani katika mkoa wa Baluchistan, mpakani mwa Afghanistan na Pakistan.

Mullah Abdul Rauf, kamanda mwandamizi wa kundi hilo amethibitisha habari hizo na kusema kuwa, Mullah Mansour aliuawa katika hujuma ya anga iliyofanywa na drone ya Marekani usiku wa kuamkia jana.

Wakati huo huo, Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan naye amethibitisha habari za kuuawa mkuu huyo wa kundi la kigaidi la Taliban. Sayed Zafar Hashemi, msemaji wa Rais Ghani amesema hujuma hiyo ilitekelezwa kufuatia makubaliano ya serikali ya nchi hiyo na Marekani na kwamba kuuawa kwa kinara huyo wa Taliban, ni mafanikio makubwa katika kufanikiwa mchakato wa kupatikana amani ya kudumu nchini humo.

Wakati huo huo, taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema kuwa, Mullah Mansour amekuwa kizingiti kikubwa cha kupatikakana amani kati ya serikali ya Kabul na Taliban na kwamba amekuwa akipanga mashambulio mengi ya kigaidi nchini Afghanistan.

Baadhi ya wanamgambo waasi wa Taliban wamepongeza kuuawa kwa Mullah Mansour na kusema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali ya Kabul kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inapatikana nchini. Kundi la Taliban lilianza kukabiliwa na mpasuko baada ya kuripuka habari za kuaga dunia kiongozi wake Mullah Muhammed Omar, Julai mwaka jana 2015. Mullah Omar aliaga dunia akitibiwa katika hospitali moja mjini Karachi nchini Pakistan, Aprili 2013.

Itakumbukwa kuwa, Washington na London zilianzisha mashambulizi makali nchini Afghanistan baada ya kujiri shambulio la Septemba 11 nchini Marekani, kwa madai kuwa magaidi wa kundi la al-Qaidah ambao walikuwa wamepewa hifadhi nchini Afghanistan walihusika katika hujuma hiyo.