Umoja wa Mataifa waonya kuhusu mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76842-umoja_wa_mataifa_waonya_kuhusu_mgogoro_wa_kibinadamu_nchini_afghanistan
Mwakilishi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Afghanistan ametahadharisha kuhusu mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoinyemelea nchi hiyo.
(last modified 2026-01-06T05:57:57+00:00 )
Nov 13, 2021 04:18 UTC
  • Umoja wa Mataifa waonya kuhusu mgogoro wa kibinadamu nchini Afghanistan

Mwakilishi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Afghanistan ametahadharisha kuhusu mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoinyemelea nchi hiyo.

Abdallah al Dardari ametoa onyo hilo katika mahojiano na tarelevisheni ya CNBC na kuongeza kuwa, kuna hatari Afghanistan ikakumbwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani. Amesema, kuna umuhimu mkubwa wa kukusanywa fedha za kuweza kusaidia kupambana na mgogoro wa kibinadamu na kutoa huduma za dharura kwa matabaka ya wananchi yaliyoko kwenye hatari kubwa zaidi.

Amesema, Umoja wa Mataifa hadi hivi sasa umekuwa ukitumia benki mbalimbali za Afghanistan na nje ya Afghanistan ambazo bado zinafanya miamala ya fedha za kigeni, kujaribu kukusanya fedha kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wa nchi hiyo.

Wanajeshi wa Marekani wakipita kwenye mashamba ya mipopi nchini Afghanistan

 

Maisha ya wananchi wa Afghanistan ni mabaya sana hivi sasa kiasi kwamba, siku chache zilizopita, shirika la habari la Sauti ya Afghani liliripoti kuwa, makadirio ya awali yanaonyesha kwamba, jumla ya hekta 224,000 za kilimo katika mikoa 22 ya Afghanistan zinatumika kwa ajili ya ulimaji wa mmea wa mpopi wa kuzalisha madawa ya kulevya.

Shirika hilo lilisema, kutokana na Marekani kuzuia mali na mitaji ya Afghanistan iliyoko nchini humo kwa kisingizio cha kupinga Taliban kushika madaraka ya nchi, hali ambayo imesababisha kuongezeka umasikini nchini Afghanistan, watu wengi wameamua kujishughulisha na ukulima wa mipopi inayozalisha mihadarati ya kasumba ili kuweza kujikimu kimaisha.

Kwa bahati mbaya ni kwamba, kukithiri ulimaji wa mipopi kumesababisha matatizo mengi kama uraibu wa madawa ya kulevya, uhalifu, kuvurugika utulivu wa kijamii, kudhoofika hali za afya za watu na kuharibika muundo wa kiuchumi wa Afghanistan.