Hizbullah yalaani vikali uamuzi wa Australia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i77282-hizbullah_yalaani_vikali_uamuzi_wa_australia
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali uamuzi wa serikali ya Australia wa kukiweka chama hicho katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusema hatua hiyo ni kujidhalilisha nchi hiyo mbele ya matakwa ya Marekani, utawala wa Kizayuni na sera za ugaidi na mauaji.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 25, 2021 04:31 UTC
  • Hizbullah yalaani vikali uamuzi wa Australia

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani vikali uamuzi wa serikali ya Australia wa kukiweka chama hicho katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusema hatua hiyo ni kujidhalilisha nchi hiyo mbele ya matakwa ya Marekani, utawala wa Kizayuni na sera za ugaidi na mauaji.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Manar, Hizbullah imetoa taarifa na kulaani uamuzi huo wa Australia na kuongeza kuwa: "Uamuzi huo na maamuzi mengine kama hayo ya baadhi ya nchi za Magharibi hayatakuwa na taathira katika moyo wa taifa tiifu la Lebanon wala moyo wa wapigania uhuru."

Hizbullah imeendelea kusema katika taarifa hiyo kuwa, "uamuzi wa Australia hautabadilisha msimamo wa harakati hiyo katika mapambano au muqawama na kuihami Lebanon na watu wake na hali kadhalika uungaji mkono kwa harakati zinazokabiliana na utawala ghasibu na vamizi wa Kizayuni."

Wapiganaji wa Hizbullah wakiwa katika gwaride

Taarifa hiyo imetolewa baada ya Australia kutangaza Jumatano kuwa imeiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Uamuzi huo wa Australia umekuja kufuatia mashinikizo ya mashirika ya Kizayuni na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa miaka kadhaa sasa Marekani na utawala wa Kizayuni zimekuwa zikifanya jitihada za kupunguza umashuhuri wa Hizbullah nchini Lebanon.