Aoun: Lebanon inahitaji Hizbullah kulinda mipaka yake
Kiongozi wa chama cha Harakati Huru ya Kizalendo nchini Lebanon (FPM) amepongeza juhudi za Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah za kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini Syria na kusisitiza kuwa, Lebanon inaiihitaji Hizbullah kulinda mipaka yake.
Michel Aoun ameiambia kanali ya televisheni ya Lebanon ya OTV kuwa, nchi hiyo inashuhudia mapigano na mashambulizi na kwamba jeshi la nchi hiyo haliwezi kuzima njama hizo kwa kuwa halina silaha na zana za kutosha.
Amesema Lebanon inaiihitaji Hizbullah ili kulinda maisha ya familia za Walebanon kutokana na hujuma za kila mara za Daesh katika mipaka yake.
Hizbullah, ambayo imesisitiza tena uungaji mkono wake kwa Aoun, imetangaza kuwa uamuzi wa kiongozi wa chama cha Vikosi vya Lebanon (LF) Samir Geagea wa kumuunga mkono kiongozi huyo wa chama cha Harakati Huru ya Kizalendo kuwa mgombea urais wa Lebanon utakuwa na taathira chanya katika kutatua hitilafu baina ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.
Tangu muda wa urais wa Michel Suleiman ulipomalizika mwezi Mei mwaka 2014 hadi sasa, kiti cha urais wa Lebanon kimebaki kitupu kutokana na mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo kushindwa kufikia mwafaka juu ya mtu atakayejaza nafasi hiyo.