Guterres: Watoto wasiopungua elfu kumi wameuawa katika vita vya Yemen
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika mkutano wa video kuhusu uchangishaji fedha kwa ajili ya Yemen kwamba takriban watoto 10,000 wameuawa katika vita vya Yemen.
Antonio Guterres amesema makumi ya maelfu ya raia, wakiwemo watoto wasiopungua 10,000, wameuawa katika vita vya Yemen na mamilioni ya wakimbizi wa ndani wanalazimika kupambana kila siku na hali mbaya ili kunusuru maisha yao.
Guterres ameongeza kuwa hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya kuisaidia Yemen na kwamba shirika la WFP limelazimika kupunguza mgao wa chakula hadi nusu kutokana na ukosefu wa bajeti.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba mgao wa chakula cha watu milioni nane umepunguzwa hivi karibuni, na kwamba suala hilo lina matokeo makubwa.
Kwa mujibu wa Guterres, katika wiki chache zijazo, takriban watu milioni nne katika miji mikubwa ya Yemen wanaweza kukosa maji safi ya kunywa, na wanawake na wasichana milioni moja wanaweza kunyimwa huduma za afya na kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia.
Umoja wa Mataifa unasema dola bilioni 4.27 zinahitajika ili kusaidia watu milioni 17.3 nchini Yemen.