HAMAS na Jihadul-Islami zawatolea mwito Wapalestina wa kushadidisha muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i81482-hamas_na_jihadul_islami_zawatolea_mwito_wapalestina_wa_kushadidisha_muqawama
Viongozi wa harakati za muqawama wa Kiislamu za Palestina za Jihadul-Islami na Hamas wametaka kushadidishwa muqawama dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2022 07:18 UTC
  • HAMAS na Jihadul-Islami zawatolea mwito Wapalestina wa kushadidisha muqawama

Viongozi wa harakati za muqawama wa Kiislamu za Palestina za Jihadul-Islami na Hamas wametaka kushadidishwa muqawama dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Mashambulio ya askari katili wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina yameongezeka katika wiki za karibuni katika maeneo mbalimbali ya Ufukwe wa Magharibi huku makundi ya muqawama ya Palestina yakisisitiza kila mara kuhusiana na jinai hizo kuwa, "muqawama wa mtutu wa bunduki" ndilo chaguo pekee la kinga ya kuzuia hujuma za adui Mzayuni.

Duru za Palestina zimeripoti kuwa, Katibu Mkuu wa Jihadul-Islami Ziyad al-Nakhala amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Hamas ukiongozwa na Naibu Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo Saleh al-Arouri katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

Katika mkutano huo, harakati hizo za muqawama za Palestina zimetoa taarifa ya pamoja zikitilia mkazo kukabiliana na uchokozi wa mara kwa mara unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi imara wa Palestina katika mji wa Quds, Ufukwe wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948.

Hamas na Jihadul-Islami zimewataka Wapalestina washadidishe muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni kutokana na jinai za kila leo zinazoendelea kufanywa na utawala huo dhalimu dhidi ya Wapalestina, ardhi zao na matukufu yao.

Halikadhlika, harakati hizo mbili kuu za muqawma za Palestina zimesisitiza juu ya kuwa tayari kwao muda wote kuulinda msikiti mtukufu wa al Aqsa na kudumisha mlingano wa nguvu uliowekwa na mapambano ya "Saiful-Quds".

Hamasa ya "Upanga wa Quds" ilishuhudiwa mwezi Mei 2021 katika makabiliano kati ya muqawama wa Palestina na utawala wa Kizayuni ambapo mamia ya makombora wa muqawama yalivurumishwa kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).../