Wazayuni 5 wauawa kwa kupigwa risasi mjini Tel Aviv
Kwa akali Waisraeli watano wameangamizwa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia leo viungani mwa mji wa Tel Aviv.
Duru za habari za Israel zimeripoti kuwa, walowezi hao wa Kizayuni waliuawa kwa kupigwa risasi na kijana wa Kipalestina katika eneo la Bnei Brak, mashariki mwa Tel Aviv.
Habari zaidi zinasema kuwa, kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 26 aliyetekeleza operesheni hiyo dhidi ya Wazayuni ameuawa pia.
Inaarifiwa kuwa, kijana huyo wa Kipalestina amefungwa jela mara kadhaa na vyombo vya usalama vya utawala wa Kizayuni, kutokana na yeye kuwa mwanachama wa harakati ya Palestina ya Fath.
Katika hatua nyingine, shirika la habari la Iran Press limeripoti kuwa, askari wawili wa jeshi la utawala haramu wa Israel wameuawa, huku wengine 12 wakijeruhiwa katika operesheni nyingine katika mji wa Al-Khadira, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Makundi ya muqawama nchini Palestina yanasisitiza kuwa, operesheni za aina hii dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni jibu kwa jinai za utawala huo pandikizi unaowaua na kuwakandamiza Wapalestina kila uchao, mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa.