Israel yawaua shahidi Wapalestina 3 siku ya kwanza ya Ramadhani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82068-israel_yawaua_shahidi_wapalestina_3_siku_ya_kwanza_ya_ramadhani
Jeshi katili la utawala haramu wa Israel limewaua shahidi Wapalestina watatu kwa kuwapiga risasi katika mji wa Jenin, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2022 08:38 UTC
  • Israel yawaua shahidi Wapalestina 3 siku ya kwanza ya Ramadhani

Jeshi katili la utawala haramu wa Israel limewaua shahidi Wapalestina watatu kwa kuwapiga risasi katika mji wa Jenin, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika la habari la Ma'an la Palestina limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Wapalestina hao wameuawa shahidi alfajiri ya leo baada ya gari lililokuwa limewabeba kumiminiwa risasi na wanajeshi wa Israel, karibu na lango la kuingia mji wa Arraba, kusini magharibi mwa Jenin.

Jeshi katili la utawala haramu wa Israel limewaua shahidi Wapalestina hao katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Baadhi ya nchi zimeanza kutekeleza ibada ya Swaum ya Ramadhani hii leo, huku nyingine zikitazamiwa kuanza kesho Jumapili.

Utawala wa Kizayuni wa Israel mbali na kuwaua shahidi Wapalestina hao, lakini pia limezuilia gari lao, sambamba na kukataa kuzipa familia miili ya mashahidi hao kwa ajili ya kuzikwa.

Katika siku za hivi karibuni, ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu imeshuhudia operesheni kadhaa za kujitolea mhanga ambapo Wazayuni 11 wameuawa.

Askari katili wa Israel wakifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi

Operesheni hizo hususan ya Jumanne iliyopita katika eneo la Bnei Brak, Mashariki mwa Tel Aviv, zimewatia hofu kubwa maafisa wa Israel, wanaohofia kwamba mashambulizi hayo yumkini yakawa mwanzo wa wimbi jipya la Intifadha na mapambano ya ukombozi ya Wapalestina dhidi ya utawala huo ghasibu.

Makundi ya muqawama ya Palestina yanasisitiza kuwa, operesheni za hivi karibuni za wanajihadi wa Kipalestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni jibu kwa jinai za utawala huo pandikizi na hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.