Al Barghuthi: Jenin haitabaki pekee yake,Wapalestina wataiunga mkono
Katibu Mkuu wa harakati ya Palestinian Initiative, Mustafa Barghouthi ameeleza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu unamwaga daumu za Wapalestina katika juhudi za kuficha kushindwa kwake kisiasa na kiusalama.
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni siku kadhaa zilizopita waliishambulia kambi ya wakimbizi ya Jenin, Kaskazini ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kuwauwa shahidi Wapalestina wanne na kuwajeruhi makumi ya wengine.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, Mustafa al Barghuti Katibu Mkuu wa harakati ya Palestinian Initiative ameshiriki katika maandamano ya kuonyesha mshikamano na raia wa Palestina wakazi wa mji wa Jenin huko Ramallah na kueleza kuwa, ukandamizaji wa Israel hautawasambaratisha Wapalestina, muqawama au irada ya raia wa ardhi ya Palestina.
Al Barghuthiamesema: "Kadhia muhimu hivi sasa ni ujumbe tunaowatumia wakazi wa Jenin kwamba tupo pamoja nao na hatutawaacha peke yao na wala hatutatoa mwanya kwa utawala ghasibu kuwazingira raia wa Kipalestina wa eneo hilo."
Makundi ya muqawama ya Palestina mara kadhaa yameeleza wazi kwamba, vita dhidi ya utawala haramu wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu viko wazi kote Palestina. Yamesema jinai za Israel haziwezi kuvuruga azma ya wananchi wa Palestina kuelekea katika njia ya mapambano kama chaguo pekee la ukombozi.