Syria: Tumejiweka tayari kukabiliana na shambulio lolote litakalofanywa na Uturuki
Wizara ya ulinzi ya Syria imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limejiweka tayari kikamilifu kukabiliana na shambulio lolote linaloweza kufanywa na Uturuki na makundi inayoyaunga mkono.
Kwa muda wa karibu miaka miwili na nusu sasa, jeshi la Uturuki limeyavamia na kuyakalia maeneo kadhaa ya kaskazini na kaskazini mashariki ya ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kupambana na magaidi na hadi sasa askari kadhaa wa jeshi la Uturuki wangaliko katika maeneo hayo.
Shirika la habari la Sputnik limeripoti kuwa, wizara ya ulinzi ya Syria imeeleza katika taarifa: "kutokana na kuongezeka harakati za Uturuki ndani ya ardhi ya Syria katika siku mbili zilizopita, tunasisitiza kuwa, jeshi limeshajiweka tayari kukabiliana na shambulio lolote linaloweza kufanywa na Ankara na magenge inayoyaunga mkono".
Wakati Uturuki inadai kwamba kuwepo wanajeshi wake kaskazini ya Syria ni kwa lengo la kuzuia vitisho vya makundi ya Kikurdi, Damascus inasisitiza kuwa hatua hiyo ni uvamizi na kukalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.
Serikali ya Syria imemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kulalamikia uamuzi uliotangazwa na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wa kutaka kufanya shambulio la kijeshi ndani ya ardhi ya Syria.../