Syria: Vikwazo ndiyo aina mbaya zaidi ya ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amevitaja vikwazo kama uhaini na aina mbaya zaidi ya ugaidi duniani.
Feisal Mekdad amesema hayo mjini Damascus katika mazungumzo yake na Meysam Latifi, Naibu Rais wa Iran na Mkuu wa Masuala ya Usimamizi na Ajira na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia kadhia ya nyuklia kwa ujasiri na mantiki.
Mekdad amelaani vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria na kueleza kuwa, sera ya vikwazo imejengeka katika misingi ya ukosefu wa maadili.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria ameongeza kuwa, taifa hilo la Kiarabu litaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Iran na kusimama na kidete na serikali ya Tehran katika kupigania haki yake ya kustafidi na teknolojia ya nyuklia.
Kwa upande wake, Mesysam Latifi, Naibu Rais wa Iran na Mkuu wa Masuala ya Usimamizi na Ajira amesisitiza juu ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili na Syria katika nyuga tofauti kwa maslahi ya wananchi wa nchi mbili hizi.
Amebainisha kuwa, Damascus na Tehran ziko makini kuchukua hatua zinazohitajika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na kutekeleza makubaliano yaliyosainiwa na mataifa haya mawili.