Msemaji wa Ansarullah aonana na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon
Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ambaye pia ni mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya wokovu wa kitaifa ya nchi hiyo, ameonana na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kujadiliana naye masuala ya karibuni kabisa ya kisiasa ya eneo hili.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la FARS ambalo limesema, Muhammad Abdul Salaam ameonana na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kujadiliana naye masuala yanayozihusu pande mbili.
Ripoti hiyo imesema, pande hizo mbili zimezungumza mambo mbalimbali lakini hasa masuala ya kisiasa ya eneo la Asia Magharibi na hususan matukio ya Yemen.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo imesema kuwa, masuala kama usitishaji vita nchini Yemen, hali halisi ilivyo nchini humo katika kila upande na mustakbali wa taifa hilo maskini zaidi la ulimwengu wa Kiarabu ni miongoni mwa masuala muhimu waliyojadiliana Katibu Mkuu wa HIzbullah ya Lebanon na msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Tuelewe kuwa, katika hotuba zake mbalimbali, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon mara nyingi amekuwa akiwaunga mkono waziwazi wananchi Waislamu wa Yemen na mapambano yao ya kukabiliana na wavamizi wa nchi hiyo wanaoongozwa na Saudi Arabia, kwa baraka kamili za Marekani na madola mengine ya kiistikbari ya Magharibi.
Kwa mfano katika moja ya hotuba zake, Sayyid Nasrullah alisema, vita vya Yemen vinaendeshwa na Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa malengo ya Marekani na njama zake dhidi ya eneo hili. Silaha ya pekee iliyobakia mikononi mwa Wamarekani na Wazayuni ni kuchochea fitina katika ukanda huu mzima lakini wananchi wa Yemen wamesimama kidete kukabiliana na njama hizo.