Sera mpya za Marekani Afghanistan
Karen Decker Kaimu Balozi wa Marekani nchini Afghanistan amesema kuwa ni jambo lililo mbali kwa nchi yake kurejea tena kijeshi huko Afghanistan.
Pamoja na hayo, Karen Decker amesisitiza suala la kuamiliana na kundi la Taliban na kutekelezwa mashinikizo kuhusu haki za binadamu kwa kundi hilo ili kuweza kutambuliwa kimataifa. Marekani ambayo mwaka mmoja uliopita iliondoka kwa fedheha huko Afghanistan baada ya miongo miwili ya kuivamia na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo katika mazingira ya kawaida ni kwamba haitorejea tena kijeshi nchini humo. Marekani ambayo inadhani itaweza kusimamia masuala ya Afghanistan kwa kuasisi vituo na kambi zake za kijeshi katika eneo hili imedai kuwa haitaingilia kijeshi masuala ya ndani ya Afghanistan.
Hii ni katika hali ambayo, kundi la Taliban linaloshikilia hatamu za uongozi Afghanistan mara kadhaa limeitahadharisha serikali ya Washington kuhusu kukiukwa anga ya Afghanistan kunakofanywa na ndege za kivita na droni za Marekani. Kwa hiyo, madai ya Kaimu Balozi wa Marekani nchini Afghanistan mwenye makazi yake huko Qatar kwamba Marekani haitaingilia kijeshi huko Afghanistan si chochote zaidi ya uwongo; bali madai hayo yana lengo la kuzipotosha fikra za waliowengi huko Afghanistan.
Akram Arefi mchambuzi wa Kiafghani anazungumzia suala hilo akisema:"Ingawa Marekani inadai kuwa imeondoka Afghanistan lakini ingali inaingilia masuala ya usalama ya nchi hiyo huku mtazamo wa Washington kwa nchi hiyo ukiwa ni mtazamo wa kujipa mamlaka ya mlinzi; mtazamo ambao unakinzana na sheria na kujitawala kwa nchi huru kwa mujibu wa kanuni za kimataifa."
Wakati huo huo Marekani inatekeleza mkakati dhidi ya Taliban kwa kustafidi na wenzo wa haki za binadamu dhidi ya kundi hilo; wenzo ambao imeutumia kwa nchi nyingine zote pinzani. Marekani inatumia wenzo wa mashinikizo dhidi ya nchi mbalimbali duniani ili kukidhi matakwa yake haramu.
Marekani hivi sasa pia si tu inatumia kama kisingizio suala la wanawake huko Afghanistan kwa ajili ya kuingilia masuala ya nchi hiyo bali inastafidi na suala hilo hilo ili kuingilia pia masuala ya ndani ya nchi nyingine duniani chini ya anwani eti ya "kutetea haki za binadamu." Hii ni katika hali ambayo ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu khususan haki za wanawake unajiri huko Marekani huku serikali ya Washington ikifumbia macho suala hilo.
Kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan ambalo sasa halina dhamira ya kuheshimu wala kutekeleza haki za wanawake na mabinti wa nchi hiyo katika sekta ya elimu limetoa kisingizio tosha kwa Marekani cha kutoa madai eti kuhusu haki za binadamu na kudai kutetea haki za wanawake na mabinti wa nchi hiyo."
Muhammad Hassan Jaafari mchambuzi wa Kiafghani anazungumzia hili akisema: Marekani si tu iliyaunga mkono makundi ya kigaidi likiwemo kundi la kitakfiri la Daesh huko Afghanistan bali imetenda jinai katika nchi nyingine na inapasa kuhukumiwa katika mahakama ya uadilifu." Pamoja na hayo, lakini Marekani bado inazungumzia kwa kiburi suala la haki za binadamu huko Afghanistan.
Ala kulli hal, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Afghanistan anajaribu kupotosha kuhusu uingiliaji mpya wa kijeshi wa nchi yake nchini humo; kwa sababu jinai za Marekani huko Afghanistan ziko wazi kikamilifu kwa wananchi wa Afghanistan huku Washington ikiendelea kuwaua Waafghani kwa mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani (droni). Aidha moja ya sera za Washington katika masuala ya Afghanistan ni uungaji mkono wa nchi hiyo kwa makundi ya kigaidi inayoyatatumia kama vikosi vya niaba. Mbali na hili, Marekani imeainisha suala la kuhamishia ugaidi kutoka Afghanistan kwenda nchi za eneo kuwa miongoni mwa sera zake za kimkakati kuhusu masuala ya ndani ya Afghanistan na ya kikanda.
Mbali na masuala ya usalama na haki za binadamu, suala la kuzuiwa fedha za Afghanistan ni jinai nyingine iliyofanywa na Marekani katika masuala ya ndani ya Afghanistan. Katika hali ambayo wananchi wa Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi; kitendo cha kuzuia karibu dola bilioni 10 za Waafghani ni pigo kubwa kwa Bodi ya Biashara na Mauzo ya Afghanistan; suala lililosababisha watoto wa nchi hiyo kuathiriwa na utapiamlo. Hii ni kwa sababu, nchi hiyo inahitaji fedha ili kununua bidhaa mbalimbali kutoka nje na shughuli za uwekezaji; fedha ambazo hata hivyo zimezuiwa na Marekani. Inachokifanya sasa Marekani ni kuwakabidhi uharibifu wananchi wa Afghanistan baada ya miongo miwili ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo.