Wakuu wa Ufaransa, Marekani na Uingereza wapuuzwa, hawakualikwa mkutano wa BRICS
Marais wa Ufaransa na Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza hawakualikwa kwenye mkutano ujao wa kundi la BRICS uliopangwa kufanyika barani Afrika.
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa akiwa mkuu wa kundi la BRICS linalojumuisha nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, ametuma mialiko kwa viongozi wa nchi 70 kushiriki katika mkutano ujao wa BRICS barani Afrika, lakini amewapuuza na kuwapa mgongo marais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Joe Biden wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sonak.
Tarehe 24 Agosti mwaka huu wa 2023, viongozi wa nchi wanachama wa BRICS watakuwa na mikutano na wakuu wa nchi 70 zilizoalikwa kwenye mkutano huo.
Afrika Kusini ndiye mwenyekiti wa sasa wa kundi la BRICS na itakabidhi uongozi wa kundi hilo kwa Russia mwanzoni mwa 2024.
BRICS ni jina la kundi linaloongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani. Kundi hili lilianzishwa mwaka 2009 katika fremu ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi wanachama kwa lengo la kukomesha utegemezi kwa sarafu ya dola ya Marekani.
Awali, Rais Vladimir Putin wa Russia alisisitiza kwamba, nchi za BRICS zinapaswa kushirikiana katika kukomesha dosari za mfumo wa fedha duniani na kufutilia mbali ulazima wa kutumia sarafu maalumu hususan dola ya Marekani kwa ajili ya miamala ya kibiashara na akiba ya kigeni.