Kukiri Marekani kuhusu kuuawa raia na ndege zake zisizo na rubani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i10420-kukiri_marekani_kuhusu_kuuawa_raia_na_ndege_zake_zisizo_na_rubani
Hatimaye serikali ya Marekani imekiri wazi kwamba, zaidi ya raia 116 wameuawa wakati wa mashambulio ya ndege zake zisizo na rubani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2016 03:42 UTC
  • Kukiri Marekani kuhusu kuuawa raia na ndege zake zisizo na rubani

Hatimaye serikali ya Marekani imekiri wazi kwamba, zaidi ya raia 116 wameuawa wakati wa mashambulio ya ndege zake zisizo na rubani.

Nyaraka zilizotolewa zinaonesha kwamba, maafa ya raia yanayotokana na mashambulio ya ndege zisizo na rubani ni mara 35 zaidi ikilinganishwa na ndege zenye rubani.

Idadi hiyo ambayo imetolewa na Mkurugenzi wa Takwimu za Kitaifa za Marekani ni ndogo ikilinganishwa na ile iliyotolewa na asasi zisizo za kiserikali. Nchini Afghanistan pekee watu 1,214 wameuawa katika mashambulio ya ndege zisizo za rubani za Marekani yaliyofanywa kwa kisingizio cha kupambana na magaidi.

Mwanzoni mwa kipindi cha uongozi wa Rais Barack Obama wa Marekani kulifanyika mashambulio 462 ya ndege zisizo na rubani katika nchi za Pakistan, Yemen na Somalia na kupelekea vifo vya raia 289. Mara zote serikali ya Obama imekuwa ikidai kwamba, ndege zisizo na rubani husababisha maafa madogo kwa raia katika vita dhidi ya ugaidi.

Hii ni katika hali ambayo, kuuawa raia kutokana na mashambulio ya ndege zisizo na rubani za Marekani kumelipua ghadhabu na hasira za wananchi kama Afghanistan, Pakistan, Yemen na Somalia.

Sartaj Aziz, mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistan katika masuala ya kigeni amesema wakati alipokuwa akizungumzia kuendelea mashambulio ya ndege zisizo na rubani za Marekani nchini Pakistan kwamba, mashambulio hayo mbali na kusababisha vifo kwa raia yanadhoofisha mwenendo wa amani wa Afghanistan.

Serikali ya Marekani inakiri kuuawa raia katika mashambulio ya ndege zake zisizo na rubani katika hali ambayo, hivi karibuni ikulu ya nchi hiyo White House ilitangaza kwamba, operesheni za ndege zake zisizo na rubani zinafanyika kwa umakini mkubwa na kwamba, eti siku zote Marekani inatambua kwamba, inapaswa kuheshimu sheria katika uwanja huo.

Afisa mmoja wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty Internation ametangaza kuwa, Marekani kwa kuendelea na mpango wake wa siri wa ndege zisizo na rubani, imetoa idhini ya kufanya mauaji na hatua hiyo ni mfano wa wazi wa jinai za kivita.

Kituo cha Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty Internation mjini Berlin Ujerumani kimetangaza kuwa, mashambulio ya ndege zisizo na rubani za Marekani katika maeneo mbalimbali ikiwemo Pakistan ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Katika hali ambayo, Marekani inatetea mashambulio ya ndege zake za kivita, idadi kadhaa ya familia za wahanga wa mashambulio hayo katika maeneo ya kikabila nchini Pakistan walikusanyika katika Kongresi ya Marekani na kutaka kusitishwa mauaji dhidi ya raia.

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu na vita dhidi ya ugaidi ametangaza kuwa, watu 2200 wameuawa nchini Pakistan na wengine zaidi ya 600 wamejeruhiwa kufuatia mashambulio 330 ya ndege zisizo na rubani za Marekani katika nchi hiyo.

Mchambuzi wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani ametathmini mashambulio ya ndege zisizo na rubani za Washington na kubainisha kwamba, kuna uwezekano mdogo mno wa kuwa na taathira amri ya Rais Obama ya kupunguzwa maafa yanayosababishwa na ndege zisizo na rubani.

Chuck Spinney ametangaza kuwa, amri ya Rais Obama ya kuchukuliwa hatua za kupunguza kiwango cha mauaji dhidi ya raia katika mashambulio ya ndege zisizo na rubani za nchi hiyo haitakuwa na taathira yoyote.

Amesema njia pekee inayoweza kupunguza mauaji hayo ni kupunguzwa idadi ya mashambulio hayo.