Holocaust halisi ya karne ya 21 yafanyika Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i105008-holocaust_halisi_ya_karne_ya_21_yafanyika_palestina
Mwakilishi wa harakati ya wanaqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas nchini Iran amesisitiza kuwa holocaust ya kweli ya karne ya 21 inajiri huko Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2023 04:18 UTC
  • Holocaust halisi ya karne ya 21 yafanyika Palestina

Mwakilishi wa harakati ya wanaqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas nchini Iran amesisitiza kuwa holocaust ya kweli ya karne ya 21 inajiri huko Palestina.

Katika kukabiliana na miongo kadhaa ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, makundi ya muqawama ya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023 yalitekeleza operesheni ya  Kimbunga cha Al-Aqsa  kutokea Ghaza dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Quds Tukufu.

Ili kulipiza kisasi na kufidia kushindwa kwake utawala huo katili ulianzisha mashambulizi ya kinyama na bado unaendelea kushambulia maeneo ya raia, hospitali na shule za Gaza na pia umefunga vivuko vyote katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Khaled Qadoumi, mwakilishi wa Hamas nchini Iran amesema katika mkusanyiko wa watu waliokutana kupinga Uzayuni na kuunga mkono Kimbunga cha Al-Aqsa uliyofanyika katika msikiti wa Imam Hussein (AS) huko Urumiyeh, Mkoa wa Azerbaijan Magharibi nchini Iran kwamba watu wa Gaza wanadhulumiwa lakini wana nguvu, na tokea Oktoba 7, walianzisha harakati ya kuuangamiza utawala wa Kizayuni na kuwapa ushindi wanyonge na kuwa siku hiyo inapaswa kupewa jina la saada kwa taifa la Imam Hussein (AS). 

Kongomano la Urumiyeh

Khalid Qadoumi ameongeza kuwa: 'Marekani baada ya kushindwa na kutengwa vikosi vyake katika eneo inaona kuwa fursa yake ya pekee ni kushiriki katika mauaji ya Wapalestina, ambapo hivi sasa Benjamin Netanyahu anawaua Waislamu kwa umati kwa kushirikiana na nchi za Magharibi zinazotoa silaha na misaada mengine kwa utawala ghasibu wa Kizayuni.'

Mwakilishi huyo wa Hamas amesema: Watoto na wanawake wanauawa kwa umati, misikiti na makanisa yanaharibiwa,  hospitali zinalengwa kwa mabomu na jinai za kutisha na dhidi ya ubinadamu zinafanyika huko Gaza huku jamii ya kimataifa ikiwa imekaa kimya.

Vahid Jalalzadeh, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Kitaifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) pia ameashiria kuwa, operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imeanda uwanja wa kuimarishwa mfungamano wa kimataifa kuhusiana na jinai za Israel huko Gaza na kuongeza: 'Utawala wa Kizayuni unajaribu kuficha kushindwa kijeshi na fedheha ya kihistoria uliyopata huko Gaza na wala hautafanikiwa katika hilo. Hamas ilitoa pigo kubwa na lisilofidika kwa ubeberu wa kimataifa.'

Mwenyekiti huyo wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Bunge  la Iran ameongeza kuwa: 'Hakuna mtu anayeweza kupuuza mauaji ya umati na ya watoto wa Palestina, na walimwengu wote wanapaswa kubainisha misimamo yao kuhusiana na jinai za kutisha zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya raia wasio na hatia.'