Dec 30, 2023 11:12 UTC
  • Hatua mpya ya serikali ya  Biden ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imetangaza kupitia taarifa kuwa imetumia mamlaka iliyopewa kisheria kuuzia utawala wa haramu wa Israel shehena ya silaha bila idhini ya wabunge wa Kongresi ya nchi hiyo.

Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amewaambia wabunge hao kuwa kwa mara ya pili mwezi huu ametumia mamlaka aliyonayo kwa ajili ya uuzaji wa dharura wa shehena ya silaha kwa utawala wa Kizayuni inayojumuisha mada zinazotumika katika kutengeneza risasi za milimita 155  zenye thamani ya dola milioni 147. Blinken Septemba 9 mwaka huu alichukua uamuzi kama huo na kukubali kuuza takriban makombora 14,000 yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 106 kwa utawala wa Israel.

Antony Blinken, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Hii ni katika hali ambayo silaha nyingi za Marekani zimetumwa Israel kwa siri tangu kuanza  vita katika Ukanda wa Gaza. Karibu mwezi mmoja uliopita, gazeti la Wall Street Journal lilifichua katika ripoti yake maalumu kuwa ili kuusaidia utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza, Marekani imeupatia utawala huo mabomu yenye nguvu kubwa ya kuvunja miamba na makumi ya maelfu ya silaha, makombora na mizinga.  Marekani ilizidisha kutuma silaha kwa utawala wa Israel unaojumuisha mabomu elfu 15 na makombora  elfu 57 muda mfupi baada ya kutekelezwa oparesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba na inaendelea kufanya hivyo hadi sasa.  

Hatua mpya ya serikali ya Biden ya kuuzatiti kwa silaha hatari utawala wa Kizayuni inaashiria masuala kadhaa. Mosi, Marekani ikiwa muungaji mkono wa Israel bila masharti yoyote hata katika hali ambayo utawala huo umeshadidisha jinai zake katika vita dhidi ya Gaza na kuwaua shahidi na kuwajeruhi maelfu ya wakazi wa Ukanda wa Gaza khususan watoto na wanawake, lakini Washington inaendelea kuunga mkono mauaji dhidi ya raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza kwa kuendeleza vita kupitia kuupatia silaha na zana za kijeshi utawala haramu wa Israel. Katika uwanja huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imeeleza kuwa nchi hiyo inabeba jukumu la kulinda usalama wa Israel na kuhakikisha kuwa utawala huo unaweza kujilinda kwa kukabiliana na vitisho vinavyoukabili; suala ambalo ni muhimu kwa maslahi ya Marekani. 

Mabomu na mizinga ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni 

Msimamo huu wa Washington unaonesha kuwa, Marekani kwa hali yoyote ile hata pale ambapo ukosoaji na malalamiko dhidi ya utawala wa Kizayuni yanazidi kuongezeka katika pembe mbalimbali duniani kutokana na jinai zake, hasa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza lakini kwa kisingizio cha kuulinda kuukingia kifua utawala huo ghasibu, inaendelea kupinga usitishaji vita huko Gaza na hivyo kuiruhusu Israel kuendeleza vita na jinai katika ukanda huo. 

Jambo la pili ni kuwa, Washington inaashiria suala la haki za binadamu huku ikiendelea kuiuzia silaha Tel Aviv ili kuendeleza mauaji dhidi ya Wapalestina. Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imedai kuwa imewasisitizia viongozi wa Israel waheshimu sheria za binadamu za kimataifa na kutekeleza hatua zote za lazima eti ili kuzuia kuwadhuru raia. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wanajua vyema kuliko mtu mwingine yoyote kwamba Israel haitambui mipaka yoyote katika vita inavyoendesha dhidi ya Wapalestina na inaamini kuwa kila hatua inayochukua ni halali yake inayopasa kukubalika na watu wote duniani. Serikali ya Biden inatambua vizuri kiwango cha jinai dhidi ya binadamu zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni lakini pamoja na hayo haijachukua hatua zozote za kivitendo ili kuzuia jinai hizo.   

Gazeti la Wall Street Journal limeandika kuhusiana na hilo kwamba: Kitendo cha kutumwa silaha za mamia ya mamilioni ya dola kwa kutumia ndege za kijeshi kutoka Marekani hadi Tel Aviv kinaonyesha changamoto za kidiplomasia zinazoikabili serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani. Kwa upande mmoja, Marekani inadai kuwa imemtaka mshirika wake huyo mkuu katika eneo aepuke kuongezeka vifo vya raia ilihali kwa upande wa pili inaipatia Tel Aviv silaha zinazotumika katika oparesheni nyingi za kijinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina.  

Upuuzaji na kutochukua hatua serikali ya Biden kumesababisha maandamano makubwa ya wananchi nchini Marekani yaliyojumuisha pia baadhi ya wawakilishi wa Kongresi ya nchi hiyo, wafanyakazi wa taasisi za serikali kama vile Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo, Wizara ya ya Usalama wa Ndani na hata wafanyakazi wa White House yenyewe. Hawa wote wanaitaka White House ichukue hatua madhubuti ili kuilazimisha Israel ikubali kusitisha vita huko Gaza. 

Maandamano ya wakazi wa New York dhidi ya mauaji ya Israel Ukanda wa Gaza 

Pamoja na hayo, serikali ya Biden inataka kutekelezwa usitishaji vita wa siku chache tu kwa ajili ya kubadilishana mateka wa Kipalestina na wa Kizayuni; na si tu inapinga kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu bali imeyapiga veto pia maazimio yote yaliyowasilishwa na nchi kadhaa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yalitaka kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza. Hatimaye Marekani ilijiepusha kulipigia kura azimio ambalo lilipendekeza kuongezwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza; azimio ambalo pia lilipingwa na utawala ghasibu wa Kizayuni. 

Tags