Feb 09, 2024 07:46 UTC
  • Ujumbe wa Bunge la Ufaransa: Israel inataka kuwaangamiza wakazi wote wa Gaza

Ujumbe wa Bunge la Ufaransa umetangaza kuwa, Israel sio tu kwamba inataka kuiangamiza Hamas, bali pia kuwaangamiza wakazi wote wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Mkuu wa ujumbe wa Bunge la Ufaransa alitangaza Jumanne iliyopita alipokuwa akitembelea kivuko cha Rafah kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza na Misri, kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kubeba jukumu la kujaribu kusimamisha vita huko Gaza.

Mkuu wa ujumbe wa Bunge la Ufaransa pia ameiomba serikali ya nchi yake kusimamisha makubaliano yote ya silaha na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa upande mwingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema: Nchi hiyo ilisimamisha leseni zote za mauzo ya silaha kwa utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba.

Katika hatua nyingine, Serikali ya Nicaragua imezishitaki Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Serikali ya Nicaragua imetangaza katika taarifa rasmi kwamba, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Canada zinahusika katika ukiukaji mkubwa na wa kimpangilio wa Mkataba wa Kuzuia na Kutoa Adhabu kwa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na Sheria za Kimataifa za Masuala ya Kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na serikali ya Nicaragua, nchi nne za Ujerumani, Uingereza, Uholanzi na Canada zimetakiwa pia ziache kupeleka silaha, risasi na teknolojia za kijeshi kwa utawala wa Kizayuni.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, kwa vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza katika hukumu yake ya Januari 26, Israel inapaswa kuhakikisha inachukua hatua zinazohitajika ili kuzuia kuendelea mauaji ya kimbari ya Wapalestina.

Katika hatua nadra kushuhudiwa, siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2024, serikali ya Afrika Kusini iliwasilisha mashtaka dhidi ya utawala wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kwamba unafanya jinai ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya Wapalestina 28,000, wengi wao wakiwa watoto, wanawake na wazee wameuawa shahidi tangu ulipoanza uvamizi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.

Tags