Mar 28, 2024 06:49 UTC
  • Francesca Albanese
    Francesca Albanese

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Palestina, Francesca Albanese, amesema kuwa amekuwa akikabiliwa na mashambulizi na kupokea vitisho vingi tangu alipoanza kazi yake ya kuandaa ripoti kuhusu jinai zinazofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Albanese amethibitisha, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ripoti yake iliyowasilishwa katika Baraza la Haki za Binadamu juu ya vita vya uharibifu vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, kwamba baada ya miezi 5 ya kuchambua mauaji yaliyofanywa na Israel huko Gaza, ripoti hizo zinathibitisha kuwepo kwa vipengele vinavyoonyesha kuwa Israel inatekeleza uhalifu wa mauaji ya kimbari huko Gaza.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: Israel inatekeleza vitendo vitatu ambavyo viko ndani ya mfumo wa mauaji ya kimbari, ambavyo ni mauaji dhidi ya Wapalestina huko Gaza, kuwafukuza kwenye makazi yao na kutengeneza hali mazingira yanayosababisha uharibifu wa sehemu au maisha yao yote.

Watoto waliouawa na Israel Ukanda wa Gaza

Francesca Albanese amethibitisha kuwa Israel inatumia silaha zilizopigwa marufuku dhidi ya Wapalestina huko Gaza na inawatesa kwa njaa, "na huu ni uhalifu wa kivita ambao haujawahi kutokea katika maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo."

Amesema kinachofanywa na Israel huko Gaza kinatengeneza mazingira ambayo yanafanya maisha ya Wapalestina yasiwezekane, na kwamba kile Israel inachofanya kinaonyesha nia yake ya kuharibu kila kitu, suala ambalo linasajiliwa kama uhalifu wa mauaji ya kimbari. 

Ripota huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa walimwengu kukabiliana na ukatili wa Israel na kuilazimisha kutii sheria za kimataifa, na kusisitiza kuwa Israel imetumia vibaya sheria za kimataifa za kibinadamu kuhalalisha ukiukaji wa haki za binadamu unaofanya huko Gaza.