Mar 30, 2024 04:31 UTC
  • Ushiriki wa Ireland katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kutokana na mauaji ya kimbari Gaza

Ireland ilitangaza Jumatano, Machi 27, kwamba itashiriki katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala wa Isarel kutokana na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo huko Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland imesema kwamba kushiriki upande wa tatu katika kesi hiyo hakumaanishi kuegemea upande wa mmoja wa wahusika, lakini ni fursa kwa Ireland kuwasilisha tafsiri yake juu ya kifungu kimoja au zaidi vya Mkataba dhidi ya Mauaji ya Kimbari (1948).

Waziri wa mambo ya nje wa Ireland, Micheál Martin, hakueleza jinsi Ireland itakavyohusika katika kesi hiyo. Katika taarifa, akiashiria jinai zinazotendwa na Israel huko Gaza amesema: "Kuchukua mateka, kuzuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu kuwafikia raia, kulenga watu na miundombinu ya kiraia, matumizi ya kiholela ya silaha na mabomu katika maeneo yenye watu wengi, matumizi ya njia za kiraia kwa madhumuni ya kijeshi, adhabu ya jumla dhidi ya raia na orodha inaendelea, ni vitendo ambavyo vinapasa kukomeshwa. Mtazamo wa jamii ya kimataifa uko wazi na hali hii haipaswi kuendelea tena."

Afrika Kusini iliishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza. Mnamo Januari, mahakama hiyo ilitangaza katika uamuzi kwamba Israeli lazima ijiepushe na hatua yoyote ambayo iko chini ya Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.

Ingawa Ireland ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na sehemu ya kambi ya Magharibi, imekuwa ikiikosoa Israel na mara kwa mara imelaani jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Leo Varadkar, Waziri Mkuu wa Ireland Jumapili, Machi 17, katika hotuba yake katika Ikulu ya White House wakati wa maadhimisho ya "Siku ya St. Patrick" na Rais Joe Biden wa Marekani, akiwa amesimama karibu naye, aliashiria historia iliyojaa mateso ya watu wa nchi yake wakati wa kupigania uhuru kutoka kwa Uingereza na akaihusisha kwa namna fulani na mapambano ya watu wa Ireland na suala la Palestina."

Leo Varadkar

Varadkar alisema: "Watu wa Ireland wana wasiwasi mkubwa juu ya maafa yanayotokea mbele ya macho yetu huko Gaza. Ninaposafiri kote ulimwenguni, viongozi mara nyingi huniuliza kwa nini watu wa Ireland wana huruma nyingi kwa watu wa Palestina. Jibu ni rahisi: tunaona historia yetu katika yale yanayojiri Gaza. Ni kisa cha kuhamishwa kwa lazima na kunyang'anywa mali, utambulisho wa kitaifa unaotiliwa shaka na kukataliwa, uhamiaji wa kulazimishwa, ubaguzi na sasa njaa."

Alisema baada ya kukutana na Biden katika Ikulu ya White House: "Nadhani hakuna hata mmoja wetu anayependa kuona silaha za Marekani zikitumiwa zinavyotumika sasa Gaza.  Njia ambazo zinatumika kwa sasa sio za kujilinda."

Jambo muhimu lililotokea baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa Ireland mjini Washington ni kujiuzulu kwake. Varadkar alitangaza Jumatano, Machi 20, katika uamuzi wa ghafla, kwamba anajiuzulu kutoka kwenye wadhifa wake kwa sababu za "kibinafsi na kisiasa". Kufuatia uamuzi huo, watumiaji wa mitandao ya kijamii walihusisha suala la kujiuzulu kwake na maneno ya dhoruba aliyotoa katika Ikulu ya White House na shinikizo la lobi ya Wazayuni ya kumuondoa madarakani.

Waziri Mkuu anayeondoka wa Ireland amekuwa akichukua misimamo imara ya kuunga mkono Palestina na kukosoa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Mwezi Novemba mwaka jana alikosoa vikali undumakuwili wa nchi za Magharibi na kusema kuwa Umoja wa Ulaya na madola ya Magharibi yanashughulikia masuala yanayohusiana na Israel na Palestina kwa undumakuwili na upendeleo wa wazi. Hatua ya  Wardkar ya kukosoa undumakuwili wa Magharibi, ukiwemo wa Umoja wa Ulaya kuhusu Israel na Wapalestina, kwa mara nyingine imeweka wazi sera za undumakuwili za Wamagharibi kuhusu masuala mbalimbali, kuanzia ugaidi na haki za binadamu hadi kadhia ya Palestina.

Kwa hakika serikali za Magharibi zimechukua misimamo ya undumakuwili katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia tu maslahi na malengo yao na wala hazijutii  kuchukua misimamo inayokinzana katika masuala mbali mbali.

Kuhusiana na suala la vita vya Gaza, mbinu hiyo hiyo ya unafiki na undumakuwili imedhihirika wazi. Ingawa nchi za Ulaya zimetoa wito wa kusitishwa mapigano mwishoni mwa mwezi wa sita wa vita vya Gaza, katika miezi ya kwanza ya vita hivyo, viongozi wa Umoja wa Ulaya walitembelea Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) ili kuunga mkono msimamo wa kijinai wa Israel wa kuendeleza vita huko Gaza kwa kisingizio cha eti kuangamiza makundi ya muqawama au wapigania ukombozi wa Palestina hususan Hamas.

Tags