Apr 05, 2024 02:19 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Russia amuonya mwenzake wa Ufaransa kutopeleka wanajeshi Ukraine

Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergey Shoygu amemuonya mwenzake wa Ufaransa Sebastian Lecornu dhidi ya kutuma wanajeshi wa nchi hiyo Ukraine.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema katika taarifa kuwa Shoygu amemueleza mwenzake wa Ufaransa katika mazungumzo waliyofanya kwa njia ya simu kwamba utekelezwaji wa mipango hiyo "utailetea matatizo hata Ufaransa yenyewe."
 
Taarifa hiyo ya wizara ya ulinzi ya Russia imeendelea kubainisha kuwa, katika mazungumzo hayo, Lecornu kwa upande wake, ametoa salamu za rambirambi kutokana na shambulio la kigaidi lililofanywa kwenye ukumbi wa tamasha wa Crocus City mjini Moscow mnamo Machi 22, na kwamba waziri huyo wa Ufaransa "amejaribu kwa kila namna kuivua Ukraine na nchi za Magharibi tuhuma za kuhusika na shambulio hilo la kigaidi na kulibebesha dhima kundi la ISIS (Daesh)."
Emmanuel Macron

Waziri wa Ulinzi wa Russia amesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea na utawabani waliohusika. Amesema: "wale wote waliohusika wataadhibiwa. Kuna athari za Ukraine katika shirika lililofanya mashambulizi ya kigaidi".

 
Aidha, Shoygu amemueleza Lecornu kwamba: "utawala wa Kyiv haufanyi chochote bila ya idhini ya wasimamizi wa Magharibi. Tunatumai kuwa katika kadhia hii, vikosi maalumu vya Ufaransa havitakuwa vimehusika".
 
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa hivi karibuni alichukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Russia kuhusiana na operesheni yake maalumu ya kijeshi iliyoanzisha zaidi ya miaka miwili iliyopita, na kuzungumzia uwezekano wa kupelekwa wanajeshi wa nchi za Ulaya huko Ukraine.../

 

Tags