Umoja wa Mataifa wabainisha 'wasiwasi mkubwa' kuhusu Israel kuua wafanyakazi wa misaada Gaza
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema limetiwa "wasiwasi mkubwa" na shambulio la anga la hivi karibuni lililofanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuua wafanyakazi saba wa shirika la misaada lenye makao yake makuu nchini Marekani.
Baraza hilo la wanachama 15 siku ya Alhamisi liliitisha uchunguzi kamili wa uwazi kuhusu tukio hilo.
Hivi karibuni utawala wa Kizayuni uliua watu saba raia wa mataifa tofauti ya Magharibi wa Shirika la Kimataifa la Mapishi (WCK) ili kuzuia misaada ya chakula kuwafikia wananchi wa Ukanda wa Gaza wanaoteseka kwa mzingiro mkubwa waliowekewa na utawala huo.
Baraza la Usalama pia lilisema kuwa Israel lazima ifanye jitihada zaidi kuboresha utoaji wa misaada katika eneo hilo lililozingirwa.
Taarifa hiyo ilitoa wito wa kuondolewa mara moja vikwazo vyote vinavyozuia utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Shirika la Kimataifa la Mapishi limesema wafanyakazi wake saba kutoka Australia, Poland, Uingereza, na raia wa Marekani-Canada waliuawa katika "hujuma ya makusudi ya Israel."
Shirika hilo lisilo la kiserikali halikuwa na hata silaha moja wakati linapeleka chakula hicho, lakini pamoja na hayo msafara wake ulishambuliwa na utawala wa Kizayuni na kukwamishwa kutekeleza kazi yake.