Apr 12, 2024 10:20 UTC
  • Kwa upinzani wa Marekani, UNSC haijaweza kufikia mwafaka wa kuipatia Palestina uanachama kamili

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) amesema, japokuwa baraza hilo limefufua matumaini ya Palestina kujiunga na Umoja wa Mataifa kwa kupatiwa uanachama kamili, lakini muafaka juu ya suala hilo bado haujaweza kufikiwa.

Balozi wa Malta Vanessa Frazier, ambaye anashikilia urais wa zamu wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Aprili amesema haukupatikana mwafaka katika mkutano wa faragha wa baraza hilo.

Frazier ameongeza kuwa, pamoja nayo, wanachama wengi walipendelea kwa uwazi kabisa kuendelezwa kampeni ya kuipatia Palestina uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Wakati kamati ya dharura ya Baraza la Usalama inaweza kupeleka mbele suala hilo kwa mwafaka wa pamoja, mwanachama yeyote wa Baraza anaweza hivi sasa kuwasilisha rasimu ya azimio ili ipigiwe kura.

Kulingana na vyanzo vya kidiplomasia, kura inaweza kupigwa Aprili 18 kupitia rasimu iliyopendekezwa na Algeria, ambayo inawakilisha mataifa ya Kiarabu katika Baraza la Usalama la UN.

Vanessa Frazier

Hata kama suala hilo litapata kura tisa zinazohitajika kati ya 15, wataalamu wa mambo wanatabiri kuwa suala hilo litakwamishwa na kura ya turufu ya Marekani.

Washington inashikilia kuwa Umoja wa Mataifa sio mahali pa kuharakisha suala la kuundwa na kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina, bali inasisitiza kwamba suala hilo inapasa litokane na makubaliano kati ya Israel na Palestina.

Palestina, ambayo tangu mwaka 2012 imekuwa na hadhi ya mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa imeshawishi kwa miaka mingi kupatiwa uanachama kamili, jambo ambalo lingekuwa sawa na kutambuliwa rasmi taifa la Palestina. 

Kwa sasa, karibu asilimia 72 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaitambua nchi ya Palestina.

Kwa mujibu wa utaratibu, ombi lolote la kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa lazima kwanza lipitie Baraza la Usalama - ambapo mshirika wa Israel, Marekani ina kura ya turufu - na ndipo kisha liidhinishwe na Baraza Kuu la umoja huo.../

Tags