Apr 15, 2024 04:28 UTC
  • Russia yakosoa kimya cha Baraza la Usalama baada ya shambulio la Israel katika ubalozi mdogo wa Iran, Syria

Russia imekosoa hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kushindwa kuchukua hatua inayofaa baada ya utawala wa Israel kushambulia jengo la ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus mji mkuu wa Syria.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia jana ilitoa taarifa ikiashiria mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Israel na kueleza kuwa, mashambulizi hayo yametekelezwa katika fremu ya kujihami na kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Hati wa Umoja wa Mataifa. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeashiria pia hatua ya jamii ya kimataifa ya kutotoa radiamali ya wazi kwa hatua iliyo kinyume cha sheria ya utawala wa Kizayuni baada ya kuushambulia ubalozi mdogo wa Iran huko Syria na kueleza kuwa, kwa bahati mbaya Baraza la Usalama la UN limeshindwa kutoa jibu linalofaa kwa utawala wa Israel baada ya shambulio la utawala huo katika eneo la kidiplomasia kutokana na misimamo ya nchi za magharibi wanachama wa Baraza la Usalama. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema inatiwa wasiwasi na kushtadi hali ya wasiwasi na ukosefu wa amani katika eneo la Asia Magharibi na kuongeza kuwa: Kutopatiwa ufumbuzi migogoro mingi katika eneo la Asia Magharibi hasa huko Palestina inayokabiliwa na mgogoro na katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ambako mara nyingi hukabiliwa na hatua za uchochezi na uibuaji machafuko kutashadidisha mivutano.  

Baada ya shambulio la utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza la  tarehe 1 Aprili katika sehemu ya ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus Syria lilowauwa shahidi washauri saba wa kijeshi wa nchi hii  huku jamii ya kimataifa ikinyamaza kimya bila ya kutoa tamko lolote la wazi la kulaani jinai hiyo ya Israel, asubuhi ya jana Jumapili Aprili 14 Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kuuadhibu utawala huo vamizi kwa kuvurumisha ndege zisizo na rubani na makombora kadhaa kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Kombora la Iran kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu 

Wakati huo huo, Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, hatua hiyo ya kijeshi ya Iran inatokana na kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi halali kwa ajili ya kukabiliana na hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya kidiplomasia vya Iran huko Damascus mji mkuu wa Syria. 

 

Tags