May 28, 2024 07:54 UTC
  • Martin Griffiths : Upuuzaji wa Israel hauwezi kuendelea; ataka kulindwa raia

Mratibu mkuu wa misaada na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya utawala wa Israel katika kambi ya wakimbizi wa ndani wa Kipalestina katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza akisema kuwa upuuzaji wa Israel hauwezi kuendelea. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka kulindwa raia na kuruhusiwa kuelekea maeneo salama.

Martin Griffiths ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni juzi usiku yameuwa makumi ya watu aghalabu yao wakiwa ni wanawake na watoto ambao wameungua wakiwa hai. 

Mratibu mkuu wa misaada na masuala ya dharura wa UN ameashiria changamoto zinazowakabili katika kusambaza misaada ya kibinadamu huko Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa: "Bado tumeshindwa kufikisha kiwango kinachohitajika cha bidhaa za mahitaji huko Kerem Shalom kufuata kuendelea mashambulizi na vita huko Gaza." 

Griffiths ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura ili kuwalinda raia na kuhakikisha usalama wao. Watu wasiopungua 45 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa shahidi na wengine karibu 250 kujeruhiwa juzi Jumapili katika mashambulizi ya anga ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo na kambi za wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Rafah.

Mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya watoto katika mji wa Rafah 

Utawala haramu wa Israel umetekeleza mashambulizi hayo tajwa katika mji wa Rafah licha ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ulioamuru Israel kusimamisha mashambulizi yake katika mji wa Rafah mara moja.

Tags