Jun 21, 2024 02:15 UTC
  • Uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu waongezeka Ulaya baada ya vita vya Gaza

Ripoti za chuki na ukiukwaji wa haki dhidi ya Waislamu zimeongezeka kwa kiwango cha kuogofya katika nchi za Ulaya tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.

Ripoti ya kila mwaka ya Kamisheni ya Kupambana na Ubaguzi ya Baraza la Ulaya iliyotolewa jana Alkhamisi imesema kuwa, kumekuwa na ongezeko la kutisha la chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu na Wapalestina katika nchi za Ulaya kufuatia mashambulio ya Oktoba 7.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, wasichana na wanawake wako katika hatari ya kunyanyaswa zaidi kwa chuki dhidi ya Uislamu, kwa sababu mavazi yao yanaweka wazi utambulisho wao wa kidini.

Kamisheni ya Kupambana na Ubaguzi ya Baraza la Ulaya imesema katika ripoti hiyo kuwa, baadhi ya nyakati, Waislamu wanabaguliwa na kunyimwa hata huduma za afya, wakilaumiwa kwa matukio yanayoendelea katika eneo la Asia Magharibi.

Ripoti hiyo imesisitiza kwamba, chuki dhidi ya wageni (xenophobia), ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi katika nchi za Ulaya, zimegeuka kuwa chuki dhidi ya Waislamu (islamaphobia) baada ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Waislamu

Uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu umeongezeka katika nchi mbalimbali duniani, baada ya kuanza kwa mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023.

Zaidi ya Wapalestina 37,400, wakiwemo watoto zaidi ya 15,500 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023, na karibu asilimia 70 ya miundombinu ya kiraia ya Ukanda huo uliozingirwa imeharibiwa.

 

 

Tags