Waandamanaji Ireland wataka kutimuliwa balozi wa Israel
Waandamanaji nchini Ireland wameandamana na kukusanyika mbele ya Bunge la nchi hiyo mjini Dublin wakitaka balozi wa utawala wa Kizayuni afukuzwe nchini humo.
Waungaji mkono hao wa Palestina wameandamana na kupiga nara kulaani jinai na mauajii ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wakiwa wamebeba mabango na maberamu, waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara dhidi ya Israel na kutoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Ireland kumfukuza nchini humo balozi wa Israel.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, idadi ya mashahidi wa vita vya mauaji ya halaiki huko Gaza yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel imekaribia 50,000.

Uchunguzi wa hivi karibuni kabisa wa Shirika la Kimataifa la Amnesty International unaonesha kuwa, utawala wa Kizayuni umefanya jinai za kutisha na unaendelea kukanyaga kikamilifu sheria na mikataba wa kimataifa.
Sehemu moja ya tamko la Amnesty International imesema: Utawala wa Israel umetumia silaha zilizopigwa marufuku kwenye mashambulio yake ya anga dhidi ya kambi ya wakimbizi huko Rafah na maeneo mengine yenye mrundikano wa raia ya Ukanda wa Ghaza.
Zaidi ya miezi 10 imepita hivi sasa tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha jinai za pande zote dhidi ya wananchi wa Ghaza huko Palestina, lakini umeshindwa kufikia malengo yake, zaidi ya kufanya jinai za kutisha za kuua kwa umati wanawake, watoto wadogo na raia wa kawaida.