Usalama kwa mtazamo wa Zarif katika Mkutano wa Munich
Malumbano ya kimadhehebu na misimamo mikali ni tishio kuu kwa eneo na ulimwengu mzima.
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria katika Mkutano wa Usalama wa Munich kuhusu ukweli huu kuwa ufumbuzi wa matatizo ya kieneo unahitajia kubadilika kigezo na mtazamo, na kuwa uhakika wa mambo.
Mkutano wa 52 wa Usalama wa Munich ulianza jana Ijumaa huko Ujerumani kwa lengo la kuchunguza migogoro ya kieneo na kimataifa kwa kuhudhuriwa na wakuu na baadhi ya viongozi wa nchi mbalimbali duniani.
Katika hotuba yake katika mkutano wa Munich, Zarif ameashiria nukta kadhaa muhimu zinazoakisi mtazamo wa Iran kuhusu usalama duniani.
Changamoto ya usalama inayoikabili dunia hivi sasa ni ugaidi na uchupaji mipaka. Ulimwengu hivi sasa unakabiliwa na tatizo la pamoja kwa jina la ugaidi; na nchi zote zinapasa kushirikiana katika uwanja huo. Hata hivyo swali linalojitokeza hapa ni hili kuwa je, mazingira ya sasa na mahusiano yaliyojaa mivutano kati ya nchi mbalimbali vitaruhusu kuwepo ushirikiano huo?
Zarif ameashiria katika sehemu ya hotuba yake kuhusu suala hilo na kueleza kuwa na hapa ninamnukuu, "sisi tunaamini kuwa hakuna kitu katika eneo letu kinachoweza kuzitenganisha nchi na kushindwa kushirikiana kwa ajili ya mustakbali mwema,"mwisho wa kunukuu.
Zarif amesema walimwengu wanakabiliwa na tishio la pamoja ambalo limeathiri hatima yao. Ameongeza kuwa hili ni tatizo ambalo watu wa Magharibi pia wanakabiliwa nalo, si kwa sababu ya wimbi la wahajiri wanaomiminika katika nchi hizo, bali kutokana na watu wanaotoka kwenye nchi hizo ambao wamejiunga na magaidi huko Syria; ambao siku moja watarejea nyumbani, jambo ambalo litakuwa ni tatizo kwa wote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia pia masuala ya eneo la Ghuba ya Uajemi ambapo amesema kuwa, wana matakwa ya pamoja na kwamba, wanataka kuona Ghuba ya Uajemi ikiwa na usalama na utulivu. Amesema suala la mafuta linapasa kudhaminiwa; na kwamba nchi zote za eneo hili zinapaswa kuwa na amani.
Kwa mtazamo wa diplomasia ya Iran, nchi za ulimwengu zina fursa ya pamoja kama ambavyo zinakabiliwa na tishio la pamoja, na kwa msingi huo zinahitajia kushirkiana ili kukabiliana na vitisho vya pamoja dhidi yao. Zarif amesema na hapa ninamnukuu, "nimaamini kuwa iwapo masuala yaliyopita yatawekwa kando, tutaweza kuanzisha kigezo kipya kwa ajili ya kushirikiana kwa pamoja kuhusu changamoto zetu, ambazo tutazishinda kwa pamoja",mwisho wa kunukuu.
Hata hivyo bado zipo nchi kama Saudi Arabia ambazo zinautazama usalama wake katika kuvuruga na kuzusha ukosefu wa amani katika nchi nyingine. Saudi Arabia inawaua kinyama wananchi wa Yemen baada ya kuanzisha uvamizi wake wa kijeshi nchini humo huku ikiendelea kuwaunga mkono kifedha na silaha magaidi ili kuing'oa madarakani serikali ya Syria. Adel al Jubair Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amezitaja harakati hizo kuwa ni sehemu ya siasa za nje za Saudia, na katika Mkutano wa Usalama wa Munich, amejaribu kuhalalisha na kutetea siasa hizo.
Hii ni katika hali ambayo chaguo pekee linalowezekana kwa ajili ya kuondokana na migogoro hii ni kushirikiana nchi zote za eneo na zisizo za eneo. Ushirikiano huo unaweza kuchukua mkondo mpana kuanzia Asia hadi Ulaya na Afrika. Iwapo hilo litawezekana, basi mazungumzo yanaweza kuanzishwa kwa mujibu wa misingi iliyokubalika kama kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi, umoja wa ardhi na nchi mbalimbali kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Katika fremu hiyo nchi mbalimbali zitaweza kuchukua hatua ili kujenga hali ya kuaminiana na hivyo kuimarisha usalama wa wote.