Utafiti: Jinai zimeongezeka katika miji mikubwa Marekani
Utafiti mpya umefichua kuwa uhalifu na jinai za kutisha zimeongeza kwa kiasi kikubwa katika miji mikubwa ya Marekani.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Major Cities Chiefs Association umeonyesha kuwa, kuna mauaji 307 zaidi yaliyofanyika katika miji mikubwa nchini humo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu 2016, ikilinganishwa na mauaji yaliyofanyika katika muda kama huo mwaka jana 2015.
Uchunguzi wa shirika hilo umebainisha kuwa, kuna visa 2,000 vya uhalifu wa kutisha, 1,000 vya wizi wa mabavu na kesi 600 za ufyatuaji risasi ovyo zilizoripotiwa katika muda huo, ambazo ni maradufu na kesi zilizoripotiwa katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka jana.
Visa vingine vinavyosemekana kuongezeka katika muda huo ni mauaji ya kifamilia na ubakaji na haswa katika miji ya Chicago, Las Vegas na Orlando.
Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita, watu zaidi ya 50 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika ufyatuaji wa risasi uliotokea katika klabu ya masenge katika mji wa Orlando jimbo la Florida nchini Marekani.