Rais Xi wa China aonya: Marekani itajitenga yenyewe
(last modified Sat, 12 Apr 2025 11:14:04 GMT )
Apr 12, 2025 11:14 UTC
  • Rais Xi wa China aonya: Marekani itajitenga yenyewe

Rais wa China, Xi Jinping ametahadharisha kuwa, Marekani iko katika hatari ya kujitenga yenyewe kwa kushupalia vita vya ushuru na vikwazo vya biashara vya upande mmoja.

Xi alitoa indhari hiyo jana Ijumaa, wakati wa safari ya Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez huko Beijing. "Hakuna washindi katika vita vya ushuru, na kusimama dhidi ya ulimwengu hatimaye kutasababisha kutengwa (Marekani)," Xi amenukuliwa na shirika la habari la Xinhua.

Xi ametoa wito kwa China na Umoja wa Ulaya "kupinga kwa pamoja uonevu wa upande mmoja" wa Marekani ili kulinda haki na maslahi yao halali, na kuzingatia sheria na utaratibu wa kimataifa.

Sera za Rais Trump za kuongeza ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini humo zimeendelea kuyumbisha biashara ya dunia.

Katika wiki iliyopita, sera hizi zimeibua dhoruba kubwa katika anga za biashara ya kimataifa. Hata hivyo, Trump amelegeza msimamo na kusema amesitisha sera hiyo kwa muda wa siku 90, ingawaje amepandisha ushuru wa bidhaa za China kwa asilimia 145.

Kushtadi vita vya kibiashara vya US na China

China imeendelea kujibu mapigo. Jana Ijumaa, ilitangaza kupandisha ushuru kwa bidhaa kutoka Marekani hadi asilimia 125, hatua ambayo imezidisha mvutano katika vita vya kibiashara kati ya mataifa haya mawili. Ushuru huo mpya uliowekwa na China dhidi ya Marekani unaanza kutekelezwa rasmi Jumamosi hii.

Rais wa China amesisitiza kuwa, bila kujali mabadiliko katika mazingira ya nje, nchi hiyo itabaki imara, yenye umakini, na itasimamia mambo yake ipasavyo.