Indhari na hatua mpya kuhusu vita vya ushuru vya Trump
Indhari na radiamali mpya zimetolewa ndani ya Marekani na kimataifa kutokana na kuendelea vita vya ushuru vya Rais Donald Trump na madai yake katika uwanja huo.
Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetahadharisha kuwa mfumo wa fedha wa kimataifa umelemewa na mashinikizo makubwa, kwa sababu vita vya kibiashara vya Rais Donald Trump wa Marekani vinavyoyumbisha masoko ya fedha. IMF imesisitiza katika ripoti yake kuwa, hatari ambazo zinatishia uthabiti wa fedha duniani zimeongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya uamuzi wa Washington wa kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa za nchi nyingine zinazoingizwa Marekani.
Wakati huo huo, kwa kuzingatia taathira mbaya za ushuru wa Trump katika masoko ya kimataifa, Mfuko wa Fedha Kimataifa (IMF) umesema ustawi wa uchumi duniani pia utapungua hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 3.3 mwaka jana. Taasisi hiyo ya fedha pia imetahadharisha kuwa kukosekana uthabiti katika mahusiano ya kibiashara kumeongezeka sana na kwamba dunia inapasa kujiandaa kwa mtikisiko zaidi wa kiuchumi, marekebisho ya bei za milki na hali ngumu ya kifedha duniani; ambapo serikali na nchi zinazoibukia kiuchumi zitarajie kushuhudia ongezeko la ghafla la gharama ikiwa ni matokeo ya hali hiyo.

Kabla ya hapo, yaani tarehe 16 mwezi huu wa Aprili pia, Shirika la Biashara Duniani (WTO) lilitahadharisha kuwa ushuru uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump utarudisha nyuma biashara ya kimataifa mwaka huu na kupelekea kushuka kwa kasi ukuaji wa uchumi wa dunia.
Katika upande mwingine, ndani ya Marekani kwenyewe pia majimbo 12 ya nchi hiyo yamefungua kesi dhidi ya utawala wa Trump katika Mahakama ya Biashara ya Kimataifa ya nchi hiyo mjini New York ili kuzuia utekelezaji wa sera ya ushuru ya Trump. Katika malalamiko yao, majimbo hayo yameeleza kuwa "sera ya ushuru ni kinyume cha sheria na imeibua hali ya wasiwasi katika uchumi wa Marekani." Majimbo hayo yaliyofungua kesi pia yamepinga madai ya Trump kwamba anaweza kutoza ushuru kiholela kwa mujibu wa Sheria ya Kimataifa ya Mamlaka ya Dharura ya Kiuchumi. Shauri hilo liliitaka mahakama itangaze ushuru huo kuwa ni kinyume cha sheria na kuzuia kutekelezwa sheria hiyo na mashirika na idara za serikali. Katika malalamiko hayo pia imesisitiza kuwa, Kongresi pekee ndio yenye mamlaka ya kutoza ushuru na kwamba Rais anaweza tu kuhuisha Sheria ya Kimataifa ya Mamlaka ya Dharura ya Kiuchumi ikiwa kutatokea hali ya dharura au tishio kuu ambalo halijawahi kushuhudia kutoka nje ya nchi.
Aprili 2, mwaka huu Donald Trump alitangaza, katika hatua isiyokuwa ya kawaida na yenye utata kutoza ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa Marekani kutoka nchi na maeneo 185 duniani. Ushuru wa asilimia10 ulianza kutumika tarehe 5 mwezi huu wa Aprili, na ushuru wa viwango vingine ulianza kutumika Aprili 9. Wakati huo huo, Trump aliongeza ushuru kwa bidhaa za China hadi asilimia125. Jumla ya ushuru unaotozwa kwa bidhaa za China sasa umefikia asilimia 145 ikiwa ni pamoja na ushuru wa ziada wa asilimia 20 uliowekwa hapo awali kwa kile Trump alichoita "uzembe wa serikali za China, Canada na Mexico katika kupambana na magendo ya fentanyl. Katika kujibu hatua hiyo ya Trump, Beijing pia ilitangaza ushuru wa asilimia 125 kwa bidhaa kutoka Marekani. Trump amelazimika kusimamisha kwa siku 90 utozaji ushuru mpya kwa nchi nyingine duniani isipokuwa China kwa kuzingatia athari mbaya za sera zake mpya za ushuru hasa hasara ya matrilioni ya dola iliyoshuhudiwa katika masoko ya hisa nchini Marekani na katika nchi nyingine.

Hii ni katika hali ambayo, kwa kuzingatia sisitizo la kutozwa ushuru mpya wa forodha inatabiriwa kuwa suala la mashirika kupata mikopo litakuwa na gharama kubwa sana kuliko hapo awali, na thamani ya pensheni na uwekezaji mwingine itapungua. Wakati huo huo, familia nyingi zitaathirika hasa ikitiliwa maanani kwamba, kadiri hali ya soko la kimataifa inavyozidi kuwa ngumu, ndivyo hatari ya kuenea mtikisiko wa kiuchumi kutoka eneo moja hadi nyingine pia inavyozidi kuongezeka.