Rais asusia duru ya pili ya uchaguzi visiwani Sao Tome
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12850-rais_asusia_duru_ya_pili_ya_uchaguzi_visiwani_sao_tome
Rais Manuel Pinto da Costa wa visiwa vya Sao Tome and Principe amesusia duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyofanyika jana Jumapili na hivyo mpinzani wake wa karibu anatazamiwa kushinda kiti hicho kiwepesi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2016 03:28 UTC
  • Rais asusia duru ya pili ya uchaguzi visiwani Sao Tome

Rais Manuel Pinto da Costa wa visiwa vya Sao Tome and Principe amesusia duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyofanyika jana Jumapili na hivyo mpinzani wake wa karibu anatazamiwa kushinda kiti hicho kiwepesi.

Rais huyo alitangaza kususia uchaguzi wa jana sambamba na kuwataka wafuasi wake wasishiriki uchaguzi huo kwa madai kuwa, duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika Julai 17 iligubikwa na wizi wa kura na uchakachuaji wa matokeo.

Evaristo Carvalho, kinara wa upinzani wa Sao Tome

Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi, kinara wa upinzani Evaristo Carvalho aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa visiwa hivyo alipata asilimia 49.8 ya kura zote halali zilizopigwa huku Rais da Costa akipata asilimia 24.8.

Rais huyo ambaye aliiongoza nchi hiyo ndogo iliyoko pwani ya magharibi mwa Afrika kwa mkono wa chuma kwa miaka 15 baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno 1975, alipoteza kiti hicho baada ya kuruhusu kufanyiwa marekebisho katiba na kuja demokrasia ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1990.

Hata hivyo alirejea ofisini baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2011. Nchi hiyo inayopatikana katika Ghuba ya Guinea ina wananchi laki mbili tu.