Iran: Undumakuwili ndio umeupa nguvu ugaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i12955-iran_undumakuwili_ndio_umeupa_nguvu_ugaidi_duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya hospitali katika mji wa Quetta nchini Pakistan na kusisitiza kuwa, usuasa za kindumakuwili ndizo zimekuza na kuzipa nguvu harakati za kigaidi katika kona mbalimbali za dunia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 09, 2016 23:19 UTC
  • Iran: Undumakuwili ndio umeupa nguvu ugaidi duniani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya hospitali katika mji wa Quetta nchini Pakistan na kusisitiza kuwa, usuasa za kindumakuwili ndizo zimekuza na kuzipa nguvu harakati za kigaidi katika kona mbalimbali za dunia.

Bahram Qasemi amesema vita dhidi ya ugaidi na misimamo ya kitakfiri na ya kufurutu ada duniani na namna baadhi ya nchi zinavyodhihirisha nyuso mbili za kukinzana katika makabiliano hayo, ambapo kwa upande mmoja zinatangaza hadharani kuunga mkono vita hivyo na kwa upande mwingine zinaunga mkono baadhi ya makundi ya kigaidi ni jambo linalohatarisha usalama wa dunia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa vita dhidi ya ugaidi na misimamo ya Kiwahabi vinaweza kufanikiwa kwa jitihada za pamoja za jamii ya kimataifa bila kuwa na misimamo ya undumakuwili.

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran

Haya yanajiri siku moja baada ya Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran kumtumia ujumbe mwenzake wa Pakistan Nasser Khan Janjua, ambapo mbali na kulaani hujuma ya kigaidi iliyofanywa katika mji wa Quetta ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Pakistan kutokana na kuuawa raia kadhaa wa nchi hiyo katika tukio hilo la kigaidi na kuzifariji pia familia za watu waliouawa.

Athari za mashambulizi ya kigaidi mjini Quetta, Pakistan

Watu wasiopungua mia moja waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika miripuko ya mabomu iliyotokea Jumatatu asubuhi katika wadi ya huduma za dharura ya hospitali moja ya mji wa Quetta ulioko kusini magharibi mwa Pakistan.