Denmark na mashinikizo ya Marekani yanayozidi kuongezeka ya kutaka kuinyakua Greenland
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135364-denmark_na_mashinikizo_ya_marekani_yanayozidi_kuongezeka_ya_kutaka_kuinyakua_greenland
Sasa hivi kuliko wakati mwingine wowote Denmark inaandamwa na mashinikizo makali ya Marekani ya kutaka kuinyang'anya nchi hiyo kisiwa cha Greenland.
(last modified 2026-01-11T05:54:27+00:00 )
Jan 11, 2026 05:54 UTC
  • Denmark na mashinikizo ya Marekani yanayozidi kuongezeka ya kutaka kuinyakua Greenland

Sasa hivi kuliko wakati mwingine wowote Denmark inaandamwa na mashinikizo makali ya Marekani ya kutaka kuinyang'anya nchi hiyo kisiwa cha Greenland.

Kwa mujibu wa Parstoday, Denmark ambayo ni miongoni mwa nchi za Ulaya mwanachama wa shirika la kijeshi la NATO na mmoja wa waitifaki wa karibu wa Marekani hivi sasa inakabiliwa na mashinikizo makubwa zaidi ya nchi hiyo ya kuitaka iipatie kisiwa cha Greenland.

Katika matamshi aliyotoa kuhusiana na suala hilo, Rais wa Marekani Donald Trump amedai, kuna ulazima wa kukichukua kisiwa cha Greenland kwa ajili ya kulinda na kudhamini usalama wa Washington na akatamka bayana kwamba, umiliki wa Greenland inawezekana ukafanyika kwa njia ya amani au kwa mabavu.

Huku akishikilia msimamo wake huo wa kwamba ni lazima Washington ikinyakue kisiwa hicho, Trump ameendelea kudai: "ikiwa hatutafanya hivyo China na Russia zitakimiliki, na sisi hatutaruhusu hilo lifanyike". Rais huyo wa Marekani ameongezea kwa kusema: "tunafanya jitihada za kuimiliki Greenland kwa sababu hatutaki China na Russia ziwe majirani zetu".

Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen (kulia) na Rais wa Marekani Donald Trump 

 

Trump ameendelea kudai kuwa, ili kudhamini usalama wake kwa njia ya kukabiliana na vitisho vya China na Russia katika katika ncha ya kaskazini ya dunia, ni lazima Marekani iwe na udhibiti wa kisiwa kikubwa zaidi duniani yaani Greenland; nayo Ikulu ya White House haijakanusha uwezekano wa Washington kutumia nguvu za kijeshi ili kukihodhi kisiwa hicho.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio yeye amelieleza jopo la wabunge maalumu wa nchi hiyo kwamba, dhamira hasa ya serikali ya Trump ni kuinunua Greenland na si kuitia mkononi kwa nguvu za kijeshi. Rubio ameyasema hayo katika kikao cha faragha cha bunge la Marekani cha kutoa ufafanuzi wa suala hilo; lakini alipokutana baadaye na waandishi wa habari alisema, tangu Trump alipoingia madarakani katika kipindi chake cha kwanza cha urais alizungumzia suala la kukimiliki kisiwa cha Greenland. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani akadai pia: "tokea hapo mwanzo, suala hilo limekuwa siku zote ndio lengo la rais. Trump si rais wa kwanza wa Marekani ambaye amechunguza au kufuatilia namna ya kuimiliki Greenland".

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kupitia tovuti ya serikali ya Greenland, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Lars Løkke Rasmussen na mwenzake wa Greenland Vivian Motzfeldt, wameomba kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani mnamo siku chacha zijazo.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Uhispania na Uingereza wametoa taarifa wakisisitiza kuwa, kisiwa hicho chenye utajiri wa madini, ambacho kinalinda njia za Aktiki na Bahari ya Atlantiki Kaskazini kuelekea Amerika Kaskazini, "ni milki ya watu wake."

Rais wa Marekani Donald Trump anapitisha muhula wake wa pili madarakani huku akionyesha waziwazi tamaa na uchu alionao wa masuala ya ardhi, biashara na fedha kwa kutaka maeneo mbalimbali ya ardhi za mataifa mengine ambayo ni washirika wa Marekani yawe sehemu ya ardhi ya nchi hiyo, pamoja na kutaka kufunga mikataba ya kibiashara itakayoipatia faida nono Washington. Katika muktadha huo, Trump anakimezea mate kisiwa cha Greenland kwa kuwa kwake eneo muhimu sana katika nchi ya kaskazini, yaani Aktiki. Kijiografia, Greenland iko kwenye eneo la kimkakati na ina rasilimali nyingi za madini. Kisiwa hicho ndio njia fupi zaidi kati ya Ulaya na bara la Amerika Kaskazini na kina umuhimu kwa mitambo ya Marekani ya kutolea onyo la makombora ya balestiki.

Serikali ya Trump imesisitiza mara kadhaa kwamba inataka kukihodhi kisiwa hicho ambacho kinamilikiwa na Denmark. Hata hivyo, viongozi wa Denmark na wa Greenland wamekuwa wakisisitiza kila mara kwamba kisiwa hicho "hakiuzwi" na wala "hakitakuwa cha Marekani."

Wagreenland wakiandamana kupinga njama ya Marekani ya kukinyakua kisiwa chao

 

Pamoja na hayo, baada ya serikali ya Trump kuishambulia kijeshi Venezuela na kumteka nyara rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro pamoja na mkewe, uwezekano wa Washington kutumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kuimiliki Greenland umepata nguvu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule. Kwa maneno mengine, ikiwa Trump hatafikia mwafaka na viongozi wa Denmark na Greenland ya kuachiwa eneo hilo kwa njia za amani, uwezekano wa Marekani kutumia nguvu za kijeshi kwa ajili ya kuimiliki Greenland utazidi kupata nguvu.../