Wakazi wa Greenland: Hatutaki kuwa Wamarekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135468-wakazi_wa_greenland_hatutaki_kuwa_wamarekani
Akthari ya wakazi wa eneo la Greenland wamesema wanahofia kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump atatekeleza kivitendo tishio lake la kulitwaa eneo hilo, wakisisitiza kuwa katu hawataki kuwa raia wa Marekani.
(last modified 2026-01-14T06:26:33+00:00 )
Jan 14, 2026 06:26 UTC
  • Wakazi wa Greenland: Hatutaki kuwa Wamarekani

Akthari ya wakazi wa eneo la Greenland wamesema wanahofia kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump atatekeleza kivitendo tishio lake la kulitwaa eneo hilo, wakisisitiza kuwa katu hawataki kuwa raia wa Marekani.

Wakazi na viongozi wa eneo hilo wanasisitiza kuwa, kisiwa hicho chenye utajiri wa madini, ambacho kinalinda njia za Aktiki na Bahari ya Atlantiki Kaskazini kuelekea Amerika Kaskazini, "ni milki ya watu wake."

"Greenland haiuzwi, na Greenland haitauzwi kamwe," Aaja Chemnitz, Mbunge wa chama cha Inuit Ataqatigiit (IA), ameiambia Al Jazeera katika mahojiano. "Watu wanaonekana kufikiria kuwa wanaweza kununua roho ya Greenland. Ni utambulisho wetu, lugha yetu, utamaduni wetu - na ingeonekana tofauti kabisa ikiwa ungekuwa raia wa Marekani, na hili si jambo ambalo wengi hapa Greenland wanalitaka."

Mbunge mwingine wa Greenland, Aki-Matilda Hoegh-Dam wa chama cha Naleraq, anasema huu ni wakati mgumu kwa wakazi 56,000 wa Greenland. Ameeleza bayana kuwa, "Vyama vyote vya Greenland vimesema kwa kauli moja kwamba hatutaki kuwa Wamarekani - na kwamba pia hatutaki kuwa Wadenmark. Tunataka kuwa Wagreenland. Tayari tuna mkoloni mmoja; hatuhitaji mkoloni mpya."

Rais wa Marekani amefufua upya takwa lake la kuhakikisha Marekani inaidhibiti Greenland, eneo la Denmark linalojiendeshea mambo yake ya ndani, akisema, Washington inahitaji kulimiliki eneo hilo ili kuzuia lisinyakuliwe na Russia na China. Trump anadai kuwa, Greenland na rasilimali zake ni muhimu kwa usalama wa taifa wa Marekani, msimamo ambao unapingwa vikali na Denmark, Greenland yenyewe na nchi za Ulaya.